Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Serikali imewataka viongozi wa mikoa na wilaya zinazopakana na nchi jirani kuongeza ulinzi na ukaguzi wa mbegu zinazoingia nchini ili kudhibiti usambazaji wa mbegu zisizo na ubora ambazo zimekuwa zikichangia malalamiko ya wakulima na kushusha tija ya uzalishaji.
Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Taifa wa Wadau wa Tasnia ya Mbegu 2026 wenye kaulimbiu ya “Kuimarisha Mfumo wa Mbegu kwa Ajili ya Usalama wa Chakula na Biashara.”
Silinde alisema baadhi ya mbegu zinazovuka mipaka huingia bila kufanyiwa ukaguzi wa kina, hali inayoweza kusababisha hasara kwa wakulima pamoja na kuathiri juhudi za serikali katika kukuza sekta ya kilimo.
Alisema ni muhimu kwa viongozi wa maeneo ya mipakani kuhakikisha mifumo ya udhibiti inakuwa imara ili mbegu zinazoingia nchini zikidhi viwango vya ubora vinavyotakiwa.
Katika hatua nyingine, aliitaka Jeshi la Magereza kuongeza uwekezaji katika uzalishaji wa mbegu zinazostahimili ukame pamoja na mbegu za mazao ya kimkakati ili kusaidia kuongeza uzalishaji wa chakula nchini.
Pia aliwataka wazalishaji wa mbegu nchini kuwekeza katika teknolojia za kuzalisha mbegu bora zinazoweza kuhimili mabadiliko ya tabianchi na magonjwa ya mazao, akisema hatua hiyo itasaidia kuimarisha viwanda vya ndani na kuongeza kipato kwa wakulima.
Kwa upande wa taasisi za kifedha, Silinde alisema kuna haja ya kuwepo kwa mikopo yenye masharti nafuu kwa wakulima na wazalishaji wa mbegu ili waweze kuwekeza katika miundombinu ya kisasa ikiwemo umwagiliaji na uchakataji wa mazao.
Alisema sekta ya mbegu ni eneo linalohitaji mtaji mkubwa hivyo ushiriki wa taasisi za fedha ni muhimu katika kufanikisha mageuzi ya kilimo.
Aidha, aliagiza halmashauri na viongozi wa serikali za mitaa kutenga maeneo maalum kwa ajili ya uzalishaji wa mbegu, akitolea mfano Wilaya ya Tanganyika ambayo tayari imetenga zaidi ya hekta 17,000 kwa shughuli hiyo.
Silinde pia aliwataka washirika wa maendeleo wakiwemo AGRA na ASPIRES kuendelea kushirikiana na serikali katika kuimarisha tafiti, sera na mifumo ya uzalishaji wa mbegu bora nchini.
Alisema serikali imeendelea kuongeza uwekezaji katika sekta ya mbegu kwa lengo la kupunguza utegemezi wa mbegu kutoka nje ya nchi huku matumizi ya mbegu bora yakiongezeka kutokana na usimamizi wa Taasisi ya Uthibitishaji Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI).
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa ASPIRES Tanzania, Profesa David Nyange alisema uzalishaji mdogo wa mazao bado ni changamoto kubwa kwa maendeleo ya sekta ya kilimo na usalama wa chakula nchini.
Alisema kiwango cha matumizi ya mbegu bora bado ni kidogo ambapo ni asilimia 34 pekee ya wakulima wanaotumia mbegu zilizoboreshwa huku matumizi ya mbegu aina ya hybrid yakiwa chini ya asilimia 10.
Nyange alisema kuna umuhimu wa kuongeza upatikanaji wa mbegu bora ili kupunguza utegemezi wa uagizaji kutoka nje pamoja na kuhakikisha mbegu zinawafikia wakulima kwa wakati.
Aliongeza kuwa pamoja na kuwepo kwa zaidi ya hekta milioni 1.5 zinazofaa kwa uzalishaji wa mbegu, ni nusu tu ya eneo hilo linalotumika kwa sasa.
Naye Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Justina Rahi alisema sekta ya kilimo bado inakabiliwa na changamoto ya uzalishaji mdogo licha ya uwepo wa ardhi kubwa ya kilimo.
Alisema Tanzania inahitaji kuongeza uzalishaji wa mbegu bora ili kukidhi mahitaji ya wakulima ambayo kwa sasa ni zaidi ya tani 130,000 huku uzalishaji ukiwa chini ya tani 80,000.
Rahi alisema gharama za mbegu bado ni kubwa kwa wakulima wengi hivyo kuna haja ya kuongeza uzalishaji ili kupunguza bei na kuwafanya wakulima wengi zaidi kuzinunua.
Alisema kutokana na matarajio ya ongezeko la idadi ya watu kufikia milioni 140 mwaka 2050, taifa linapaswa kuwekeza zaidi katika uzalishaji wa mbegu bora kwa ajili ya kuhakikisha usalama wa chakula unakuwepo kwa muda mrefu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TOSCI, Nyasebwa Chimagu alisema taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 yanafikiwa kupitia sekta imara ya mbegu.




Social Plugin