
Kwa miongo kadhaa, wananchi wa Jimbo la Ukerewe wamepata changamoto kubwa ya kukosa mawasiliano ya usafiri hasa nyakati za usiku, hali ambayo imechochea kudhoofika kwa uchumi wa wananchi wa maeneo hayo kwa kukosa fursa za mwingiliano wa kibiashara na wilaya na mikoa jirani.
Kwa kutambua changamoto hiyo, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia bajeti ya Wizara ya Ujenzi iliyowasilishwa Mei 21, 2026 na Waziri mwenye dhamana ya wizara hiyo Mhe. Abdallah Hamis Ulega, bunge lilipitisha shilingi trilioni 2.564 kwa mwaka wa fedha 2026/2027 ndani yake ikiwepo ujenzi wa daraja jipya linalounganisha Ukerewe - Kisorya, Bunda.
Hatua hiyo imeibua hisia zilizojaa furaha kwa wananchi wa jimbo hilo ambao kwa miongo kadhaa walijiona kuwa kifungoni kwa kutokuwepo na miundombinu ya daraja katika kivuko cha Kisorya - Ukerewe hali iliyochochea kukosekana kwa mawasiliano kati ya Ukerewe na mikoa jilani.
Katika bajeti hiyo, Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi inayosimamiwa na Waziri Mhe. Abdallah Hamis Ulega kwa kusaidiwa na Naibu wake Eng. Godfrey Kasekenya imetangaza kuanza rasmi kwa mradi huu.
Daraja hilo lenye urefu wa kilometa 0.9 litajengwa kwa awamu mbalimbali kwa gharama ya shilingi bilioni 250 ili kuunganisha wilaya ya Ukerewe na Bunda katika kivuko cha Kisorya - Ukerewe.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Ukerewe ambaye pia ni Naibu Waziri, Dkt. Switbert Zacharia Mkama, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na bunge kwa kupitisha bajeti hiyo ambayo inakwenda kutibu changamoto za wananchi zilizowakosesha amani kwa miongo kadhaa.
"Kiupekee nampongeza sana Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutatua shida na changamoto za kutokuwepo kwa usafiri wa uhakika Ukerewe, Wananchi waliishi kama kifungoni hasa inapofika nyakati za usiku, hapakuwepo na mawasiliano ya daraja ambalo lingechochea kukuza uchumi wao kwa mwingiliano wa wafanyabiashara kutoka mikoa jirani" Alisema Dkt. Mkama
Aidha, Dkt. Mkama amesema upatikanaji wa daraja hilo utasaidia kuinua uchumi wa mwananchi kwa kufanya biashara muda wote, pia wananchi wagonjwa wanaopewa rufaa, itasaidia kuokoa maisha yao kwa kupata matibabu ya haraka kupitia uwepo wa daraja hilo" Alisema
"Ujenzi huu utasaidia kuinua mapato na kukuza uchumi wa wananchi kwa kurahisisha usafirishaji wa bidhaa mbalimbali na kuokoa maisha ya wananchi hasa wagonjwa, jambo ambalo hadi sasa mtu akizidiwa usiku tunatumia gharama kubwa ya Ambulance boti, hivyo tunampongeza sana Mhe. Rais" Alisema
Pia, Dkt. Mkama amempongeza Waziri wa Ujenzi Mhe. Abdallah Hamis Ulega kwa kusaidiwa na Naibu wake Eng. Godfrey Kasekenya kwa kazi kubwa wanayoitekeleza katika kuhakikisha wananchi wa jimbo la Ukerewe wanaondokana na changamoto hiyo ili kukuza uchumi, na uhusiano wa kijamii baina ya jamii jilani na wilaya hiyo.
"Daraja hilo pia litaimarisha mahusiano ya kiukoo, umoja, amani na mshikamano kati ya jamii za Ukerewe na jamii za mkoa wa Mara kwa kutambua undugu uliopo katika maeneo hayo" Alisema
Pamoja na mambo mengine, mradi huo unatarajia kuifungua Ukerewe na kuwa kitovu cha Utalii, biashara, na wananchi kupata maendeleo makubwa kiuchumi.




Social Plugin