Na Hadija Bagasha Tanga,
Aliyekuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama cha National League for Democracy (NLD) Doyo Hassan Doyo, amevitaka vyama vya siasa nchini kuacha siasa za mihemko na badala yake kuzingatia sheria, taratibu na kanuni zinazosimamia usajili na uendeshaji wa vyama vya siasa ili kulinda amani na utulivu wa Taifa.
Aidha Doyo amesema hatua ya Msajili kuiandikia barua Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuomba ufafanuzi kuhusu kauli ya mmoja wa viongozi wake ni ishara kuwa sheria inasimamiwa kwa usawa kwa vyama vyote vya siasa nchini.
Kwa mujibu wa Doyo, hatua hiyo imeongeza matumaini kwa wananchi na wadau wa siasa kwamba hakuna chama kitakachopewa upendeleo mbele ya sheria.
Doyo ambaye ni Katibu Mkuu wa chama hicho, ametoa kauli hiyo akizungumza na waandishi wa Habari jijini Tanga, kuhusu mwenendo wa siasa nchini, ambapo alisisitiza kuwa hakuna chama, mwanasiasa au mwanaharakati anayepaswa kujiona yupo juu ya sheria huku akiitaka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuendelea kusimamia sheria bila woga wala upendeleo.
“Kuna wanaharakati na wanasiasa ambao wanajiona wapo juu ya sheria na wana uwezo wa kusema chochote huku wakitishia Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa wakisahau kuwa ofisi hiyo ipo kisheria na iko imara,” alisema Doyo.
Aidha, aliitaka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuendelea kuchukua hatua kwa vyama au viongozi watakaobainika kwenda kinyume na sheria bila kuangalia ukubwa wa chama husika au ushawishi wake wa kisiasa.
Kwa mujibu wa Doyo, taasisi yoyote inayosimamia sheria inaposhindwa kutekeleza wajibu wake kwa wakati, hujenga mazingira ya sintofahamu, migogoro na kuporomoka kwa nidhamu ya kisiasa nchini.
“Tutakapokuwa na taasisi ambayo haina uwezo wa kushughulikia matatizo ya jambo inalolisimamia, kitakachokuja ni maafa na uvunjifu wa amani ndiyo maana tumejitokeza mbele ya Watanzania kueleza kuwa kila upande unapaswa kuwajibika kwa mujibu wa sheria,” alisema.
Katika hatua nyingine, Doyo aliipongeza Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa kile alichodai kuwa ni uthubutu wa kuchukua hatua kwa vyama mbalimbali vya siasa bila upendeleo.
Akizungumzia hatua zilizochukuliwa dhidi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), alisema pamoja na kuwepo kwa malalamiko na mjadala mkubwa wa kisiasa, chama hicho hatimaye kilitoa majibu kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kama ilivyotakiwa kisheria.
“Msajili aliwatandika barua CHADEMA wakahangaika nayo, lakini mwisho wa siku wameijibu na kupeleka maelezo yao. Hii inaonyesha kuwa sheria lazima ifuatwe,” alisema.
Pia alisema hatua ya Msajili kuiandikia barua Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuomba ufafanuzi kuhusu kauli ya mmoja wa viongozi wake ni ishara kuwa sheria inasimamiwa kwa usawa kwa vyama vyote vya siasa nchini.
Kwa mujibu wa Doyo, hatua hiyo imeongeza matumaini kwa wananchi na wadau wa siasa kwamba hakuna chama kitakachopewa upendeleo mbele ya sheria.
“Tumeona Msajili amekichukulia hatua pia Chama Cha Mapinduzi kwa kukiandikia barua ili nao watoe maelezo ya kina kuhusu kauli za viongozi wao. Hii inaongeza matumaini makubwa kwa vyama vya siasa pamoja na wananchi kwa ujumla,” alisema.
“Tuna matumaini hata CCM watawasilisha majibu yao kwa Ofisi ya Msajili hivyo tunaendelea kuipongeza ofisi hiyo kwa sababu haijaogopa kuchukua hatua kwa taasisi yoyote ya kisiasa,” alisema.


Social Plugin