Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WANAUME KALENGA WAVUNJA UKIMYA, WAAPA KUTOKOMEZA UKATILI WA KIJINSIA


Na Deogratius Temba,Iringa

Wanaume katika Kata ya Kalenga, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, wamejitokeza hadharani kuvunja ukimya na kuapa kupambana na ukatili wa kijinsia, kufuatia mdahalo maalum ulioratibiwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP).

Mdahalo huo, uliofanyika chini ya mradi wa “Kuvunja Vikwazo:

 Kupambana na Ukatili wa Kijinsia,” uliwakutanisha Wanaume zaidi ya 60 na wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa kimila, dini, serikali na vyombo vya dola, ukilenga kuwahusisha wanaume moja kwa moja katika mapambano dhidi ya vitendo hivyo.

Akizungumza katika mdahalo huo, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Saumu Kweka, alisema:

“Ukatili wa kijinsia hauhusu wanawake pekee; ni jukumu la jamii nzima.
 Wanaume wakisimama imara kulinda familia, tutapiga hatua kubwa katika kuutokomeza.”

Kwa upande wake, Polisi kata, Mkaguzi wa Polisi, Editha Kayuni, alisisitiza umuhimu wa wananchi kutoa taarifa kwa wakati:

“Jeshi la Polisi lipo tayari kushughulikia vitendo vya ukatili bila upendeleo. Tunawasihi wananchi kuvunja ukimya na kushirikiana nasi ili sheria ichukue mkondo wake.”

Akichangia mjadala huo, Afisa Mtendaji wa Kata ya Kalenga, Loveness Kinyunyu, alisema mdahalo huo umeleta mwamko mpya:

“Elimu hii imewafungua wanaume wengi. Sasa wanatambua kuwa wanaweza kuwa sehemu ya suluhisho kwa kuanzia ngazi ya familia.”

Naye kiongozi wa kimila, Meshaki Masange, alikemea mila potofu zinazochochea ukatili:
“Kuna baadhi ya desturi zimepitwa na wakati. Ni wajibu wetu kuzibadilisha ili kulinda heshima na usalama wa wanawake na watoto.”

Makamu Mwenyekiti wa Kituo cha Taarifa na maarifa, kata ya Kalenga, Peter Mvula, aliongeza kuwa wanaume wana nafasi kubwa ya kuleta mabadiliko:

“Mabadiliko ya kweli yataanza pale wanaume watakapochukua hatua ya kubadili mitazamo yao na kuwajibika katika familia na jamii.”

Katika mdahalo huo, wanaume walikiri kuwepo kwa vitendo vya ukatili na kuahidi kuwa mabalozi wa mabadiliko. 

Walikubaliana kutumia majukwaa ya kijamii kuelimishana, kupinga mila kandamizi, na kushirikiana na vyombo vya dola kuhakikisha sheria zinatekelezwa.

Mdahalo huo umeacha ujumbe mmoja ulio wazi mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia hayawezi kufanikiwa bila ushiriki wa wanaume. 

Kupitia elimu na dhamira ya pamoja, jamii ya Kalenga imeanza safari ya kujenga mazingira salama, yenye usawa na heshima kwa wote.

Moja ya mafanikio makubwa ya mdahalo huo ni kuwafanya wanaume kufunguka na kujadili masuala ambayo mara nyingi hubaki gizani. 

Washiriki walieleza kwa uwazi uzoefu wao, wakikiri kuwepo kwa vitendo vya ukatili ndani ya jamii zao, na baadhi yao hata kukiri kuwa wahanga wa ukatili wa kijinsia.

 Kupitia mjadala huo, waliweza kuunganishwa na Dawati la Jinsia la Polisi ili kupata msaada na mwongozo wa kisheria, hatua inayochochea ujasiri wa kutoa taarifa na kufuatilia haki.

Katika maazimio yao, wanaume hao walikubaliana kuanza mabadiliko kutoka kwao wenyewe kwa kuwa mabalozi wa kupinga ukatili wa kijinsia. Walisisitiza kutumia majukwaa ya kijamii yanayowakutanisha wanaume, kama vile vijiwe vya kahawa, michezo ya bao na mikusanyiko ya kijamii, kuelimisha wenzao kuhusu madhara ya ukatili huo. 

Pia walikubaliana kupinga mila na desturi potofu zinazochangia vitendo hivyo, pamoja na kushirikiana na vyombo vya dola kuhakikisha sheria zinazingatiwa.

Kwa kuzingatia sheria na miongozo iliyopo nchini, ikiwemo Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 na Sheria ya Makosa ya Kujamiiana (SOSPA), ni wazi kuwa serikali imeweka msingi imara wa kupambana na ukatili wa kijinsia. Hata hivyo, utekelezaji wake unategemea ushiriki wa jamii, hususan wanaume, katika kubadili mitazamo na kutoa ushirikiano kwa mamlaka husika.





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com