Wakazi zaidi ya 100 wa Kitongoji cha Kibosha Mji Mpya wamejitokeza kuomba kuunganishiwa huduma ya majisafi na salama, wakati mradi wa maji wa Kibosha Mnarani ukiendelea kukamilishwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA).
Mwitikio huo mkubwa umetokana na fursa iliyotolewa na Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire, inayowawezesha wananchi kupata maunganisho ya maji kwa mfumo wa kulipa kidogo kidogo hadi watakapokamilisha malipo, hatua inayolenga kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma hiyo muhimu kwa haraka.
Akizungumza wakati wa zoezi la kupokea maombi ya wateja wapya, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano DAWASA, ndugu Everlasting Lyaro, amesema tangu kutangazwa kwa ofa hiyo katika maeneo yaliyopitiwa na mradi, mwitikio umekuwa mkubwa, huku wananchi zaidi ya 110 wakijitokeza kuomba kuunganishiwa huduma ya majisafi.
“Kwa muda mrefu wananchi wa Kibosha walikuwa na changamoto kubwa ya maji kwa kuwa eneo hili halikuwa na mtandao kabisa. Utekelezaji wa mradi huu umehamasisha wengi kujitokeza kuomba kuunganishiwa huduma,” amesema Lyaro.
Ameongeza kuwa hadi sasa maombi ya wateja wapya yamevuka 100, huku zoezi la kuwaunganisha likiendelea sambamba na hatua za mwisho za kukamilisha mradi huo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kibosha, ndugu Shabani Athuman, amesema mradi huo utaleta mageuzi makubwa kwa wananchi, hasa kwa kuondoa utegemezi wa maji ya visima yasiyo salama na safari ndefu za kutafuta maji.
“Tunamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea mradi huu kupitia DAWASA. Awali tulikuwa tukitegemea visima vilivyokuwa mbali na maji yake hayakuwa salama. Sasa tunapata huduma bora karibu nasi,” amesema Athuman.
Naye mkazi wa Kibosha Area B, Bi. Zubeda Saidi, amesema uwepo wa huduma ya maji pamoja na mfumo wa kulipa kidogo kidogo ni faraja kubwa kwa wananchi waliokuwa wakikabiliwa na adha ya muda mrefu ya ukosefu wa majisafi.
“Tunashukuru sana maji yamefika. Hii fursa ya kulipa kidogo kidogo imetusaidia sana, ndiyo maana tumejitokeza kujiandikisha kwa wingi,” amesema Zubeda.
Mradi wa maji wa Kibosha Mnarani, uliowekewa jiwe la msingi na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, ndugu Wazo Mwang’onda, unagharimu shilingi milioni 182.5 huku ukilenga kuhudumia kaya 500 katika vitongoji vya Area A, Area B na Area C, na unatarajiwa kuondoa kabisa changamoto ya maji katika eneo hilo.
Kwa sasa, DAWASA inaendelea na zoezi la kuunganisha wateja wapya sambamba na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya maji, taratibu za maunganisho pamoja na huduma nyingine muhimu, ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha huduma ya majisafi inawafikia wananchi kwa ufanisi na endelevu.




Social Plugin