Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TUME YASHAURI ELIMU ZAIDI KWA WATANZANIA KUELEWA YANAWASIBU

 

TUME ya Rais ya Kuchunguza Vurugu za wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 imeshauri mambo matatu ikiwemo kutoa elimu kwa Watanzania kuzuia matukio kama hayo ili kuendeleza amani na utulivu wa nchi.

Makamu Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Mkuu mstaafu Profesa Ibrahim Juma alisema hayo jana wakati tume ilipokutana na wahariri na waandishi wa Habari kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere.

Alisema ili kila Mtanzania aweze kujua ukweli kuhusu mambo yanayoendelea nchini, kuna umuhimu wa kuwa na mkakati maalum wa mawasiliano utakaotoa nafasi ya kila mwananchi kupata taarifa sahihi kutoka katika vyombo mbalimbali vya habari.

Aidha, alieleza kuwa nafasi ya mitandao kuwa jukwaa la kujadili amani na usalama wa nchi haitekelezwi kikamilifu hivyo kushauri kuwepo kwa mwongozo wa elimu ya namna ya kutumia yanayopatikana katika mitandao kwa sababu wapo wanaoamini kila picha mjongeo zinazopita katika mitandao.

“Mitandao hii imetawaliwa na watu maarufu ambao watakachoongea kinachukuliwa kama kilivyo kama ukweli wenyewe. Hii hutoa mwanya wa kuvumisha uzushi na kuleta taharuki ndani ya nchi kwa jambo ambalo sio la kweli,” alieleza Jaji Profesa Juma.

Alisema tume ilitafuta wataalamu wa kuzichunguza taarifa za mitandaoni hususani picha mjongeo ili kujua ipi ni ya kweli na isiyokuwa ya kweli akitolea mfano wa baadhi ya matukio waliyogundua kuwa yalitokea katika nchi za nje lakini yanatajwa kuwa ni ya Tanzania.

Alisisitiza kuwa ni jambo jema kuona tume ikikosolewa katika vyombo vya habari akisema itawezesha tume kufanya kazi kwa mafanikio na kuviasa vyombo vya habari kujikita katika kutoa taarifa zenye kusaidia umma na taifa kwa ujumla.

“Jambo ambalo tumelibaini katika kukosolewa, kuna wale wanakosoa bila kuwa na uwezo wa kuelewa. Wanategemea wengine wanaochanganua na kuyafuata yale wanayoyasema na tumeona hiyo ni hatari sana hasa kwa Tanzania,” alisisitiza

Aliongeza kuwa watu wengi hawasomi magazeti kusikiliza redio wala kufuatilia televisheni za ndani wanategemea mitandao ambayo haiwapi elimu itakayowawezesha kujua kinachotokea katika nchi yao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com