Na Mwandishi Wetu
Jaji Mkuu Msitaafu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema kuwa kuundwa kwa Tume huru ya Uchunguzi wa Matukio ya Vurugu zilizotokea kabla na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 ni taswira nzuri ambayo nchi imeonesha kuwa inao uwezo wa kushughulikia na kutatua changamoto zake yenyewe bila kuingiliwa na watu wa nje.
Prof. Ibrahim amesisitiza kuwa Tume hiyo ni huru na haingiliwi na Taasisi au mtu mwingine wa nje na ni tume ya Kimataifa kwani inaongonzwa na sheria za Kimataifa na sio za Tanzania pekee na imesheheni watu wabobevu wenye uzoefu wa kazi za Kimataifa.
Alieleza wazi kuwa tume hiyo iko huru na haiingiliwi na taasisi yoyote, jambo linaloipa nguvu ya kufanya maamuzi kwa kuzingatia ukweli, ushahidi na maslahi mapana ya taifa bila shinikizo la nje.
Aidha, Prof. Juma alibainisha kuwa tume hiyo imesheheni wabobezi kutoka katika fani mbalimbali, wenye uzoefu mkubwa na uelewa mpana wa masuala wanayoyashughulikia. Alisema uwepo wa wataalamu hao ni msingi imara unaoihakikishia jamii kuwa kazi zote zinafanyika kwa viwango vya juu vya kitaalamu.
Katika msisitizo wake, alieleza kuwa uwezo wa ndani uliopo unatosha kabisa kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii.
“Tunaambia dunia kuwa tuna uwezo wa kushughulikia changamoto zetu wenyewe kwa kutumia rasilimali watu na utaalamu tulionao,” alisisitiza Prof. Juma.
Kauli hiyo inaakisi dhamira ya kujitegemea na kujiamini kwa taasisi za ndani katika kusimamia masuala muhimu ya kitaifa, huku ikiimarisha taswira ya nchi katika jukwaa la kimataifa.

Social Plugin