Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TANCCOOPS YAZINDUA MAGARI MAPYA 6 KURAHISISHA USAFIRISHAJI



Muungano wa Vyama vya Ushirika vya Pamba nchini (TANCCOOPS) umetumia kiasi cha shilingi bilioni 1.55 kununua magari sita mapya, ikiwa ni mkakati wa kupunguza gharama za uendeshaji na kurahisisha usafirishaji wa mazao ya wakulima.

Hafla hiyo ya uzinduzi wa magari imefanyika, April 10, 2026 katika ofisi za TANCCOOPS Mkoani Shinyanga. 

Akizungumza kwenye hafla hiyo Mwenyekiti wa TANCCOOPS, William Leonard Lyambagwa, amesema uamuzi huo umekuja baada ya kubaini kuwa wanatumia gharama kubwa kukodi makampuni binafsi ya usafirishaji kwa ajili ya shughuli za kilimo na biashara.

“Kabla ya kutekelezwa kwa mradi huu, tumekuwa tukitumia fedha nyingi kulipa makampuni ya nje. Magari haya yatatusaidia kuongeza ufanisi, na tuna mpango mkakati wa kuongeza mengine zaidi ili kutanua wigo na kufikia malengo tuliyojiwekea,” amesema William Lyambagwa.

Said Tangawizi, kutoka Chama Kikuu cha Ushirika Mbogwe na Bukombe (MBCU), amesema kuwepo kwa usafiri wa uhakika kutasaidia wanachama kupata mbolea na mbegu za kupanda kwa wepesi na wakati muafaka tofauti na hapo awali huku Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika Mkoa wa Simiyu, Mohamed Matani, akiongeza kuwa hatua hiyo ni mapinduzi makubwa katika sekta ya pamba yatakayomsaidia mkulima wa chini kupata huduma bora.

Akihitimisha hafla hiyo, Mgeni Rasmi ambaye ni Naibu Mrajis wa Vyama vya Ushirika, Collins Nyakunga, ametoa rai kwa wanachama na viongozi kuhakikisha wanasimamia uendeshaji wa mradi huo kwa uadilifu mkubwa huku akisisitiza utunzaji wa vitendea kazi hivyo ni nyenzo muhimu itakayohakikisha mradi unakuwa endelevu na unaleta tija ya kiuchumi kwa wanaushirika wote.




















Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com