Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania Sheikh Dkt. Abubakar Zubeir Bin Ally ameonesha kuridhishwa na utendaji wa Tume huru ya kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani wakati na baada ya uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2026, akibainisha kufurahishwa na weledi wake katika utekelezaji wa shughuli zake kulingana na hadidu za rejea zilizowasilishwa kwa tume hiyo.
Sheikh Zubeir Bin Ally ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Aprili 13, 2026 wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar Es Salaam, akisema kuundwa kwa tume hiyo ilikuwa wazo na fikra sahihi katika kudumisha amani, umoja na kuponya majeraha yaliyotokea wakati wa uchaguzi.
"Tume hii ipo sawa sawa sana katika muktadha wa haki na maridhiano ya Kitaifa na nina matarajio makubwa kutokana na tume ile kwani ina uwezo na weledi mkubwa katika utekelezaji wa majukumu yake na Tume hii itatuweka pazuri kwani lilikuwa wazo na fikra sahihi za kuundwa kwa Tume hii kwani ninaamini itaponya majeraha na kuleta pozo na matokeo makubwa katika nchi yetu." Amesema Sheikh Mkuu.
Aidha Kiongozi huyo amesisitiza Tume hiyo kusimama imara katika kusimamia haki na kuhakikisha maridhiano yanafikiwa, akihimiza zaidi umuhimu wa majadiliano katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto za kisiasa na kijamii pamoja na wananchi kutatua matatizo yao wenyewe badala ya kutaka watu kutoka nje ya nchi kuja kutatua changamoto za ndani ya nchi.

Social Plugin