Waheshimiwa Madiwani wakiwa katika ziara ya kutembelea mradi wa maji uliopo mtaa wa Mahilo kata ya Matogoro Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma lengo kuu kuwajengea uelewa madiwani kuhusu mipango ya muda mfupi na mrefu ya kuboresha huduma ya maji
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma Abraham Egno Mbunda akizungumza na waheshimiwa madiwani baada ya kukamilika kwa zoezi la ziara ya kutembelea mradi wa kimkakati wa maji wa miji 28 kata ya Matogoro Na Regina Ndumbaro Songea-Ruvuma
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Songea (SOUWASA), Mhandisi Patrick Kibasa, leo Aprili 13, 2026 ameongoza ziara ya waheshimiwa madiwani pamoja na watumishi wa SOUWASA kutembelea mradi wa kimkakati wa maji wa miji 28 unaotekelezwa katika Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma.
Katika ziara hiyo, Kibasa ameeleza kuwa lengo kuu ni kuwajengea uelewa madiwani kuhusu mipango ya muda mfupi na mrefu ya kuboresha huduma ya maji, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya pande hizo mbili.
Akizungumza katika ziara hiyo, Kibasa amesema madiwani ni wawakilishi wa wananchi hivyo ni muhimu wafahamu kwa kina shughuli na mipango ya mamlaka hiyo ili waweze kuwasilisha mahitaji ya wananchi ipasavyo.
Ameongeza kuwa kupitia kikao hicho, madiwani wametoa maeneo ya kufanyiwa kazi na SOUWASA, huku mamlaka hiyo ikitarajia ushirikiano wa karibu ili kuhakikisha huduma bora ya maji inawafikia wananchi wote.
Aidha, Kibasa amebainisha kuwa madiwani hao wamepata fursa ya kipekee ya kutembelea mradi mkubwa wa maji ambao awali walikuwa wakiusikia bila kuushuhudia.
Ziara hiyo imewawezesha kuona hatua iliyofikiwa, maendeleo yake pamoja na changamoto zinazoukabili, jambo litakalosaidia kuongeza uwajibikaji na ufuatiliaji wa karibu wa miradi hiyo muhimu kwa maendeleo ya Manispaa ya Songea.
Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea, Abraham Egno Mbunda, amewataka madiwani na menejimenti ya SOUWASA kuendeleza umoja, ushirikiano na mashauriano ili kulinda maslahi ya wananchi.
Pia ameipongeza SOUWASA kwa kutoa mawasilisho yaliyoeleweka, huku akisisitiza umuhimu wa viongozi kutembelea miradi ili kujionea hali halisi badala ya kutegemea maelezo pekee, hasa katika maeneo yenye changamoto za upatikanaji wa maji.
Naye akizungumza kwa niaba ya madiwani wenzake, Diwani wa Kata ya Mjimwema Silvester Mhagama pamoja na Diwani wa Kata ya Mshangano Benson Sovella wameipongeza SOUWASA kwa juhudi zake na ziara hiyo yenye tija.
Wamesema mradi wa maji wa miji 28 utaleta mabadiliko makubwa kwa wananchi, hasa katika maeneo ya pembezoni yaliyokuwa yakikumbwa na changamoto ya maji.
Wameongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo, unaoungwa mkono na uwekezaji mkubwa wa Serikali, kutasaidia kuondoa kero ya maji na kuboresha maisha ya wakazi wa Manispaa ya Songea.







Social Plugin