Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BEROYA YAWEKA HISTORIA MPYA UFAULU WA ASILIMIA 100

Mheshimiwa Diwani wa Kata ya Mshangano Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma Benson Sovella akimkabidhi muhitimu wa kidato cha sita cheti katika shule ya Sekondari Beroya katika hafla ya Mahafali yaliyofanyika leo shuleni hapo 


Meneja wa Shule za Beroya John Waryuba wa pili kulia akiwa pamoja na mgeni rasmi na viongozi wengine katika hafla ya Mahafali yaliyofanyika leo tarehe 25 aprili 2026 shuleni 

Na Regina Ndumbaro Songea-Ruvuma 

Mahafali ya kumi na sita ya kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Beroya, iliyopo Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, yamefanyika leo tarehe 25 aprili 2026 kwa mafanikio makubwa huku yakibeba ujumbe mzito wa kuhimiza bidii, ushirikiano na maadili kwa wanafunzi. 
Mgeni rasmi katika hafla hiyo, Mheshimiwa Diwani wa Kata ya Mshangano, Benson Sovella, amewapongeza walimu kwa kazi yao ya kujitolea licha ya changamoto wanazokutana nazo, akiwahimiza kuendelea kufanya kazi kwa moyo huo huo ili kuendeleza mafanikio ya shule na jamii kwa ujumla.

Akizungumza katika hafla hiyo, Sovella Ameeleza kuridhishwa na maendeleo ya shule hiyo katika sekta mbalimbali ikiwemo miundombinu ya umeme, maji, maktaba na huduma za afya, akiahidi kuwa balozi mzuri wa kutetea na kuendeleza jitihada hizo. 

Aidha, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wazazi, walimu na uongozi wa shule ili kuhakikisha wanafunzi wanapata matokeo bora zaidi, huku akiwataka wahitimu kujiandaa vyema kwa maisha yajayo kwa kumtanguliza Mungu na kufanya kazi kwa bidii.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Beroya, Ludovick Mkumbae, amesema kuwa shule hiyo imepiga hatua kubwa tangu kuanzishwa kwake mwaka 2007, ikikua kutoka wanafunzi 46 na walimu 6 hadi kufikia wanafunzi 231 na walimu 18 kwa sasa. 

Ameongeza kuwa shule imeendelea kufanya vizuri kitaaluma kwa kupata ufaulu wa asilimia 100 katika miaka ya 2024 na 2025, pamoja na kusajili mtaala mpya wa lugha ya Kichina na kuimarisha mazingira ya kujifunzia kwa vitendo, ikiwemo uwepo wa maktaba kubwa, chanzo cha maji, nishati jadilifu na zahanati.

Hata hivyo, Mkumbae ametaja changamoto zinazoikabili shule hiyo kuwa ni pamoja na ulipaji hafifu wa ada, ushiriki mdogo wa wazazi katika shughuli za shule na ucheleweshwaji wa wanafunzi kurejea shuleni baada ya likizo. 

Ameeleza mikakati iliyowekwa kukabiliana na hali hiyo, ikiwa ni pamoja na kuongeza ufaulu wa daraja la kwanza, kuboresha miundombinu na mazingira ya shule pamoja na kutoa huduma bora za afya kwa jamii inayozunguka shule hiyo.

Naye Meneja wa Shule za Beroya, John Waryuba, amewahakikishia wazazi kuwa dhamira yao ni kuhakikisha kila mwanafunzi anapata mafanikio bora bila kujali changamoto za mazingira, akisisitiza kuwa lengo ni kuifanya Beroya kuwa shule bora kitaifa.
 
Kwa upande wa wahitimu, mwanafunzi Veronica Jackson Ndunguru, aliyefanikiwa kupata vyeti vitatu katika masomo ya sayansi, amebainisha kuwa siri ya mafanikio yake ni juhudi binafsi, nidhamu ya kusoma kwa bidii, kumtanguliza Mungu na kushirikiana kwa karibu na walimu wake.
Wahitimu wa kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Beroya iliyopo Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma 


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com