Imeelezwa kuwa amani ni miongoni mwa rasilimali muhimu zinazohitajika kuanzia kwenye ngazi ya Familia hadi Taifa ili kufanikisha jitihada mbalimbali za maendeleo zinazofanywa na mtu mmoja mmoja, jamii na Taifa kwa ujumla, wito ukitolewa kwa kila Mtanzania kuwa mstari wa mbele katika kulinda na kudumisha amani.
Wakizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar Es Salaam leo alhamisi Aprili 16, 2026, baadhi ya wananchi akiwemo Bi. Stella Mlawa Mkazi wa Ilala, amesema amani pia ndiyo inayozalisha upendo na mshikamano wa jamii na familia, akikiri kuwa ikiwa amani itapotea malezi kwenye ngazi ya familia yatakuwa mabaya na uchumi wa Taifa utayumba, huku pia maendeleo yakishindwa kufikiwa.
"Amani ni hali ya utulivu, ikivurugika tu nyumbani malezi yanakuwa mabaya, kitaifa maendeleo na uchumi utayumba. Muhimu tuilinde amani yetu, tutumie mitandao ya kijamii kwa manufaa ili isiwe chanzo cha kuvuruga amani yetu." Amesema Bi. Mlawa.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama cha michezo ya jadi Tanzania Bw. John Nguchiro amesema amani na michezo ni vitu vyenye kuhusiana kwa karibu huku kila kimoja kikiimarisha kingine, akisema michezo hustawi zaidi katika mazingira yenye utulivu na amani ndio chombo chenye kukuza umoja, mshikamano na maelewano miongoni mwa watu wenye asili na utamaduni tofauti.
Bw. Nguchiro ameeleza pia mchango wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika utunzaji wa tunu muhimu za Taifa, akieleza namna ambavyo aliitumia michezo kuunganisha jamii na kukuza amani huku pia akimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo ameendelea kuhakikisha kuwa Taifa linasalia lenye amani, umoja na mshikamano.

Social Plugin