
Wakati Watanzania wakitarajia kupokea ripoti ya Tume ya Kuchunguza Matukio ya Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 baadae leo , ni dhahiri kuwa amani, umoja wa kitaifa, na maridhiano si tu misingi ya kijamii, bali ni mahitaji ya lazima kwa ukuaji wa uchumi wa nchi.
Kwa sasa, maeneo mengi barani Afrika yanakumbwa na misukosuko ya kisiasa ambayo imesababisha kudorora kwa uwekezaji, kuyumba kwa sekta ya utalii, na kusimama kwa miradi ya maendeleo. Kwa kuzingatia hali hiyo, Tanzania inapaswa kuichukulia ripoti hii si kwa jicho la kisiasa pekee, bali kama dira ya kulinda mustakabali wa kiuchumi, kwani utulivu ukikosekana, gharama ya kuurejesha itakuwa kubwa na imani ya wadau wa maendeleo inaweza kupotea kwa haraka.
Takwimu za hivi karibuni za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na mashirika ya kimataifa kama IMF, zinaonyesha kuwa uchumi wa Tanzania uko katika mwelekeo chanya, ukiwa na ukuaji wa Pato la Taifa unaokadiriwa kufikia asilimia 5.9 na mfumuko wa bei wa wastani wa asilimia 4.0 kwa mwaka 2026. Hizi ni ishara za uchumi imara unaopaswa kulindwa kwa nguvu zote dhidi ya misuguano ya ndani isiyo ya lazima. Aidha, akiba ya fedha za kigeni iliyofikia Dola za Marekani bilioni 6.244 inatosha kuagiza bidhaa nje kwa miezi mitano, kiasi ambacho kimejenga kinga muhimu dhidi ya majanga ya kiuchumi ya kimataifa, hivyo kinga hizo hazipaswi kuchezewa na mifarakano.
Mifano kutoka nchi jirani barani Afrika inatoa somo tosha kuhusu athari za ukosefu wa amani ambapo nchini Sudan, kuporomoka kwa utulivu kulisababisha mfumuko wa bei kufikia asilimia 180 na kuvuruga kabisa mfumo wa uzalishaji. Hali kadhalika, Ethiopia imekumbwa na changamoto ya uendelevu wa deni kutokana na migogoro, huku Msumbiji ikipoteza uwekezaji mkubwa katika mkoa wa Cabo Delgado kutokana na uasi. Hata nchini Kenya, ghasia za uchaguzi wa mwaka 2007/08 zilisababisha mapato ya utalii kuporomoka kwa asilimia 60, jambo linalothibitisha kuwa sintofahamu ya kisiasa inagusa maisha ya mwananchi wa kawaida kupitia kupotea kwa ajira na kupanda kwa gharama za maisha.
Sekta ya utalii nchini Tanzania, ambayo ilichangia mapato ya safari ya takribani Dola bilioni 4.3 kufikia Februari 2026, inategemea zaidi taswira ya nchi kuwa tulivu na inayotabirika. Bajeti inayopendekezwa ya mwaka 2026/2027 ya Shilingi trilioni 62.3, ambapo asilimia 74.2 inategemea mapato ya ndani, ni uthibitisho mwingine kuwa mipango ya maendeleo na kujitegemea inajengwa juu ya msingi wa utulivu. Hivyo, ukomavu wa serikali na busara za viongozi katika kupokea ripoti hii ni muhimu katika kuwapa uhakika wakopeshaji, wawekezaji, na wananchi ili waendelee kujitoa kwa ajili ya maendeleo ya taifa kwa muda mrefu.
Social Plugin