Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAJIPANGA KUZIFANYIA UKARABATI SHULE ZOTE KONGWE NCHINI - PROF. SHEMDOE



Na OWM – TAMISEMI, Dodoma

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI, Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, amesema Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI imeandaa andiko la mradi unaoitwa SIFA yaani (School Infrastructure Facelifting Programme) na kuliwasilisha Wizara ya Mipango, ili kuwezesha upatikanaji wa fedha za kufanyia ukarabati wa shule zote kongwe za awali, msingi na sekondari nchini.

Prof. Shemdoe amesema hayo Aprili 15, 2026 wakati akijibu hoja za Waheshimiwa Wabunge walizoziwasilisha wakati wa kujadili Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka 2026/27.

“Namshukuru Mheshimiwa Prof. Kitila Mkumbo na timu yake ya Wizara ya Mipango kwa kulipokea andiko tulilowasilisha ili tupate fedha za kutekeleza mradi wa ukarabati wa shule kongwe nchi nzima,” amesema Prof. Shemdoe.

Prof. Shemdoe amefafanua kuwa, tathmini iliyofanyika imebaini ukarabati unahitajika kwenye shule za msingi ikihusisha vyumba vya madarasa ni 42,716 na nyumba za walimu 31,813 na kwa upande wa shule za sekondari inajumuisha vyumba vya madarasa 6,889, nyumba za walimu 3,518, maktaba 91 na mabweni 309. 

Prof. Shemdoe ameanisha kuwa, Serikali imekuwa ikitoa fedha kwa ajili ya kufanya ukarabati kwa awamu ambapo kati ya mwaka 2021/22 hadi 2025/26, Serikali imetumia shilingi bilioni 237.9 kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa miundombinu mipya ya shule za msingi na Sekondari kongwe na chakavu nchini.





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com