Na Jackline Minja, WMJJWM,MBEYA
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi, amewataka wadau mbalimbali mkoani Mbeya kuendelea kushirikiana na kituo cha kulea watoto wenye usonji cha Funguka Foundation kilichopo Kata ya Ilomba, ili kusaidia juhudi za malezi na huduma kwa watoto wenye mahitaji maalum.
Mhe. Mahundi ametoa wito huo alipofanya ziara katika kituo hicho Machi 07, 2026.
Amesema kazi ya kulea na kuwahudumia watoto wenye mahitaji maalum ni jukumu la pamoja la jamii, hivyo kuna umuhimu wa wadau mbalimbali kujitokeza kusaidia vituo vinavyotoa huduma hizo.
“Ni muhimu kwa wadau na jamii kwa ujumla kushirikiana kusaidia vituo kama hivi. Kazi inayofanywa hapa ni kubwa na ya kipekee kwa kuwa inahusisha kuwalea na kuwahudumia watoto wenye mahitaji maalum. Tunapaswa kumuunga mkono meneja wa kituo hiki ili awe na nguvu zaidi ya kuendelea kutoa huduma bora kwa watoto hawa,” amesema Mahundi.
Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Nassirya Nassir Ally amesema ataendelea kulisimamia suala la watoto wenye mahitaji maalum ili kuhakikisha wanapata huduma wanazostahili.
Amesema watu wanaojitoa kuwahudumia watoto hao wanatoa mchango mkubwa kwa jamii na taifa kwa ujumla, hivyo wanastahili kuungwa mkono na kuthaminiwa.
“Nitahakikisha suala la watoto wenye mahitaji maalum linaendelea kupewa kipaumbele ili waweze kupata huduma stahiki.
"Nawapongeza sana wale wanaojitoa kuwahudumia watoto hawa kwani wanatoa mchango mkubwa kwa jamii na Taifa.” Amesema Nassir Ally.
Naye Meneja wa kituo cha Funguka Foundation Nelly Elisha ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kuendelea kukisaidia kituo hicho kwa mahitaji muhimu na kuwafikisha wadau wanaochangia maendeleo ya kituo hicho.
Aidha, mmoja wa wazazi wa watoto wanaolelewa katika kituo hicho, Bi. Zulfa Abdul Lyimo ameipongeza Serikali kwa juhudi zake za kuwajali watoto wenye mahitaji maalum na kuahidi kuendelea kushirikiana na kituo hicho ili kuhakikisha wanapata malezi bora na fursa za maendeleo.



Social Plugin