
KATIKA kile kinachoonekana ni kuongezeka kwa imani ya jumuiya ya kimataifa kwa Serikali ya Awamu ya Sita, Mfuko wa Pamoja wa Afya (Health Basket Fund) umetajwa kuwa muhimili mkuu uliogusa maisha ya mamilioni ya Watanzania, huku ukiingiza zaidi ya dola za Marekani bilioni 1.3 (takriban Shilingi trilioni 3.4) tangu kuanzishwa kwake.
Akizungumza Machi 2, 2026, jijini Dar es Salaam katika mkutano wa kimkakati na washirika wa maendeleo, Waziri wa Afya, Mhe. Mohammed Mchengerwa, amesema ushirikiano huo umekuwa chachu ya mageuzi makubwa, hususan katika kuimarisha huduma za afya ya msingi zinazosimamiwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Waziri Mchengerwa amebainisha kuwa tangu mwaka 2017, serikali ilifanya mapinduzi ya kiutawala kwa kupeleka fedha moja kwa moja kwenye vituo vya afya 7,345 nchi nzima, hatua iliyoongeza uwazi na kupunguza urasimu wa kutoa huduma kwa wananchi.
Akielezea mwelekeo wa sasa, Mhe. Mchengerwa amesema Tanzania ipo kwenye kipindi cha mpito kuelekea utekelezaji kamili wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote. Alisisitiza kuwa mfumo wa kidijitali uliounganishwa (Integrated Digital Health) ndio utakuwa "macho na masikio" ya serikali katika kupima ufanisi wa huduma.
“Huwezi kusimamia usichokiona, na huwezi kuboresha usichokipima. Mfumo wa kidijitali ni mageuzi ya utawala, ufanisi na uaminifu katika sekta yetu,” alisema Waziri Mchengerwa.
Katika hatua inayolenga kupunguza utegemezi wa nje, Waziri ameweka wazi kuwa serikali sasa inaangazia uzalishaji wa ndani wa dawa na vifaa tiba. Alifafanua kuwa suala la upatikanaji wa bidhaa za afya si la kiuchumi pekee, bali ni suala la usalama wa afya ya Taifa, hivyo serikali inajipanga kuwa na ustahimilivu wa dharura za kiafya.
Akizungumza kwa niaba ya timu ya mabalozi na wadau wa maendeleo, Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Mhe. Elke Wisch, amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa ujasiri na kazi kubwa katika kupunguza vifo vya akina mama na watoto.
Mhe. Wisch alihitimisha kwa kuiahidi serikali kuwa washirika wa kimataifa wataendelea kuchangia kwenye mfuko huo kutokana na kuridhishwa na namna fedha zinavyotumika kwa uwazi na kuleta matokeo chanya katika vituo vya afya kote nchini.
Social Plugin