Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BALOZI MIGIRO ASHUSHA NYUNDO: CCM NI URITHI WA UKOMBOZI, WANAOBEZA WANA SHIDA YA UFAHAMU

KATIKATI ya minong’ono ya kisiasa na kejeli za mitandaoni zinazojaribu kupotosha ukweli, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Asha-Rose Migiro, ametoa dongo zito kwa wanaobeza nafasi ya chama hicho katika harakati za ukombozi wa Afrika.

Akifungua kikao cha kimkakati cha Makatibu Wakuu wa Vyama Rafiki vya Ukombozi Kusini mwa Afrika (FLM) huko Kibaha, mkoani Pwani jana Machi 4, 2026, Dkt. Migiro amesisitiza kuwa CCM si chama cha siasa cha kawaida, bali ni taasisi iliyobeba vinasaba vya ukombozi wa bara hili.

Kauli hiyo imekuja kufuatia kuibuka kwa baadhi ya watu wanaojaribu kufuta historia ya CCM kama chama kiongozi katika harakati za kumng'oa mkoloni kusini mwa Afrika, jambo ambalo wadadisi wa mambo wamelitafsiri kama "ushamba na mhemuko wa kijinga" usiozingatia historia ya nchi.

Dkt. Migiro, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere (MJNLS), amesema kuwa kuanzia mwaka 2026 hadi 2030, vyama vya ukombozi vimejipanga kuimarisha malezi ya kiitikadi kwa vijana ili wasiyumbishwe na mabadiliko ya kiteknolojia.

"Chuo hiki si kituo cha mafunzo pekee, ni uwekezaji wa kudumu katika kuishi falsafa ya Mwalimu Nyerere. Tunajenga viongozi wenye uzalendo na uelewa wa changamoto za karne ya 21," alisema Dkt. Migiro.

Akielezea uzito wa eneo la chuo hicho kilichopo Kibaha, karibu na Bagamoyo, Balozi Migiro amekumbusha kuwa eneo hilo lina uzito wa kipekee kihistoria kwani lilikuwa kitovu cha harakati za ukombozi. Amesema kupuuza nafasi ya CCM katika mnyororo huo ni kukosa uelewa mpana wa safari ya mataifa ya Kusini mwa Afrika kuelekea uhuru.

Kikao hicho cha siku mbili kinashirikisha vinara wa siasa barani Afrika ikiwemo: CCM (Tanzania).ANC (Afrika Kusini)FRELIMO (Msumbiji) , MPLA (Angola) naWAPO (Namibia).

Lengo kuu ni kurejesha misingi ya ukombozi kwa kada na viongozi chipukizi, huku wakiboresha mifumo ya kidijitali kukabiliana na vita vya kisaikolojia na propaganda zinazoenezwa dhidi ya vyama vya ukombozi.

Wakati sehemu ndogo ya watu ikijaribu kupiga kelele mitandaoni kuhusu uhalali wa CCM kama chama cha ukombozi, historia inasimama upande wa CCM. Ni dhahiri kuwa "kujichetua" kwa hali ya kutoijua historia hakuwezi kufuta ukweli uliowekwa kwa jasho na damu na waasisi wa mataifa haya.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com