
Na Kadama Malunde – Malunde 1 Blog
Hifadhi ya Msitu wa Lubaga maarufu kama Hashi ni kielelezo cha uzuri wa asili, ikiwa na miti mizuri, mandhari ya kipekee, na vivutio vinavyotoa burudani na elimu kwa wageni.
Hivi sasa, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Wilaya ya Shinyanga wanaendelea kuboresha mazingira hayo kwa ujenzi wa vivutio mbalimbali, huku wakitarajia kuzindua rasmi utalii wa ikolojia ifikapo Julai mwaka huu.
Utalii huu wa ikolojia unalenga kutoa fursa mbalimbali ikiwamo kupiga picha, kupumzika, na kushirikisha hafla za harusi pamoja na sherehe nyingine, huku pia ukichangia elimu ya uhifadhi wa mazingira.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 20, 2026, Ofisa Mwandamizi wa Uhifadhi kutoka TFS Wilaya ya Shinyanga, Fabian Balele, amesema: “Hifadhi ya Lubaga ina vivutio vya asili vinavyovutia watalii, hivyo tumeanza kuweka miundombinu ya msingi kwa ajili ya shughuli hizo.”
Balele ameainisha baadhi ya huduma zinazotarajiwa kuanzishwa ambazo ni pamoja na utalii wa ikolojia ukiwamo kupiga picha na kupumzika, kumbi za mikutano ya nje kwa hafla mbalimbali zikiwamo harusi, njia ya baiskeli yenye urefu wa kilomita saba, pamoja na bustani ya wanyama itakayowezesha watalii kufurahia uzuri wa asili.
Aidha, watalii watakaotembelea eneo hilo watapata elimu ya uhifadhi wa misitu na ufugaji wa nyuki, jambo linalosaidia kulinda na kuhifadhi mazingira.
Hifadhi ya Lubaga inatarajiwa kuwa kivutio cha kipekee cha utalii wa ndani, kikichangia burudani, elimu, na fursa za kiuchumi kwa wananchi na wageni.
















































Social Plugin