Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ELIMU YA TAKUKURU YAINUA MAPATO USHETU; VIFAA VYA UJENZI VYA MILIONI 51.7 VYAOKOLEWA MSALALA


Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Donasian Kessy

Na Kadama Malunde, Shinyanga

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Shinyanga imesema elimu dhidi ya rushwa iliyotolewa kwa watumishi wa sekta ya afya na wadau wa mapato katika Halmashauri ya Ushetu imechangia kwa kiasi kikubwa kuimarika kwa ukusanyaji wa mapato ya ndani, huku mapato yakiongezeka kwa asilimia 366 kwa mwezi.

Akitoa taarifa ya robo ya pili ya mwaka wa fedha (Oktoba–Desemba 2025) leo Machi 4, 2026, Mkuu wa TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Shinyanga, Donasian Kessy, amesema mafunzo ya maadili, uwajibikaji na madhara ya rushwa kwa watumishi wa afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu yameleta mabadiliko chanya katika utendaji kazi.

“Kupitia mafunzo na elimu iliyotolewa na TAKUKURU kuhusu maadili na uwajibikaji na madhara ya rushwa kwa watumishi wa afya Halmashauri ya wilaya ya Ushetu, uadilifu umeimarika na kupelekea ufanisi mkubwa katika utendaji kazi wa sekta hiyo. Awali kulikuwa na malalamiko mbalimbali ya upotevu wa mapato na huduma isiyoridhisha wananchi,” amesema Kessy.

Amefafanua kuwa kabla ya utoaji wa elimu hiyo, Idara ya Afya ilikuwa ikikusanya wastani wa shilingi milioni 3 kwa mwezi, lakini baada ya maboresho mapato yameongezeka hadi kufikia shilingi milioni 14 kwa mwezi , ongezeko la shilingi milioni 11 sawa na asilimia 366.

Kwa mujibu wa Kessy, ongezeko hilo limechangia kuboresha huduma za afya katika vituo vya kutolea huduma, kupunguza malalamiko ya ucheleweshaji wa huduma na kuongeza imani ya wananchi kwa watumishi wa sekta hiyo.

Katika hatua nyingine, TAKUKURU imefanikiwa kuokoa vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya shilingi 51,752,600/= baada ya kubaini kuwa mzabuni alinunua vifaa hivyo bila kuviwasilisha katika mradi wa ujenzi wa nyumba ya mtumishi katika Shule ya Msingi Magongwa, Halmashauri ya Wilaya ya Msalala.

Kessy amesema kwa ujumla taasisi hiyo imefuatilia miradi 18 ya maendeleo yenye thamani ya shilingi 3,536,123,370/= katika kipindi hicho, hatua iliyosaidia kuimarisha uwajibikaji na kulinda fedha za umma.

Aidha, TAKUKURU imefanikiwa kudhibiti ukwepaji wa ushuru wa mazao katika Manispaa ya Shinyanga kwa kuimarisha doria kwenye maeneo ya ukusanyaji ushuru. Uchambuzi wa awali ulibaini kuwepo kwa mianya ya ukwepaji kupitia mageti kwa kutumia njia zisizo rasmi.

Katika robo hiyo, TAKUKURU ilipokea jumla ya malalamiko 39, ambapo 22 yalihusu tuhuma za rushwa na 17 hayakuhusu rushwa na yalielekezwa kwenye mamlaka husika. Pia kesi mbili mpya za rushwa zilifunguliwa mahakamani huku kesi moja ya zamani ikiendelea kusikilizwa.

TAKUKURU imesisitiza kuwa itaendelea kutoa elimu kwa watumishi wa umma na wananchi ili kuimarisha uwajibikaji, hususan katika sekta nyeti kama afya ambako uadilifu una mchango mkubwa katika kulinda mapato ya serikali na kuboresha huduma kwa wananchi.

TAKUKURU inatoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za vitendo vya rushwa kupitia namba ya bure 113 ili kuunga mkono juhudi za kupambana na rushwa mkoani Shinyanga.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com