
KATIKA kile kinachoonekana kuwa ni mkakati kabambe wa Serikali ya Awamu ya Sita kuimarisha misingi ya umoja na utulivu wa kitaifa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Clement Sangu, amefanya ziara ya kihistoria katika Ofisi za Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) jijini Dar es Salaam.
Ziara hiyo iliyofanyika Februari 19, 2026, imelenga siyo tu kujitambulisha, bali kuweka bayana jukumu jipya na nyeti la kuratibu mahusiano nchini ambalo ofisi yake imekabidhiwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kama injini ya kuendesha amani na maendeleo jumuishi kwa Watanzania wote.
Akipokelewa na Mwenyekiti wa JMAT, Dkt. Alhad Mussa Salum pamoja na baraza la wajumbe wa jumuiya hiyo, Mhe. Sangu ametoa pongezi za dhati kwa taasisi hiyo kwa kuwa kimbilio na nguzo muhimu ya maadili inayohimiza maridhiano na uvumilivu miongoni mwa waumini wa dini mbalimbali
Waziri amebainisha kuwa juhudi za JMAT zimekuwa chachu ya kudumisha utulivu wa kitaifa ambao ndio msingi wa kila hatua ya kimaendeleo nchini. Amesisitiza kuwa bila kuwepo kwa mahusiano mema na mshikamano wa kijamii, juhudi nyingine za kiuchumi na kisiasa zinaweza kukwama, hivyo kuitaja JMAT kama mshirika wa kimkakati wa serikali katika ujenzi wa taifa.
Aidha, katika mazungumzo hayo yaliyojaa hamasa, Mhe. Sangu ameweka uzito wa kipekee kwenye hitaji la ushirikiano wa karibu kati ya serikali na taasisi za kidini katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii kwa sasa.
Ameeleza kuwa masuala ya malezi bora na mmomonyoko wa maadili yanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza ili kutengeneza kizazi chenye nidhamu na uzalendo. Kwa mujibu wa Waziri Sangu, serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha kuwa ajenda ya amani inavuka mipaka ya maneno na kuwa vitendo, ikihusisha nyanja za kijamii, kiuchumi, na hata za kikanda na kimataifa ili kulinda mustakabali wa nchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa JMAT, Dkt. Alhad Mussa Salum, ametoa shukrani za dhati kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wake wa busara wa kuanzisha Wizara mahsusi inayoshughulikia mahusiano, hatua ambayo ameiita kuwa ni utambuzi wa hali ya juu wa mahitaji ya jamii ya sasa.
Dkt. Alhad amemhakikishia Waziri Sangu kuwa jumuiya yake itaendelea kuwa bega kwa bega na serikali katika kuhakikisha kuwa umoja wa kitaifa hautikisiki. Alihitimisha kwa kusema kuwa kuthaminiwa kwa mchango wa taasisi za kidini katika kurekebisha mienendo ya jamii ni ishara ya uongozi uliotukuka unaolenga kuijenga Tanzania imara na yenye maridhiano ya kweli.

Social Plugin