Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI, SEKTA BINAFSI ZAUNGANISHA NGUVU KUTULIZA KIU YA AJIRA



KATIKA hali inayolenga kupunguza changamoto ya ajira kwa vijana nchini, Serikali imetoa wito kwa sekta binafsi kuendelea kushirikiana nayo katika kubuni mifumo inayotoa fursa halisi za kiuchumi badala ya kusubiri ajira za rasmi pekee.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Mhe. Deus Sangu, wakati wa uzinduzi wa jukwaa jumuishi la kitaifa la “IMBEJU – Bongo Fursa Show”, lililoandaliwa na Taasisi ya Benki ya CRDB kwa kushirikiana na Chama cha Kitaifa cha Biashara na Maendeleo (NEDC).

Waziri Sangu alisema kuwa vijana ni kundi kubwa linalohitaji kushirikishwa kikamilifu katika mikakati ya kujenga uchumi wa taifa, na kwamba jitihada za sekta binafsi kama Benki ya CRDB ni mfano wa kuigwa katika kutafsiri maono ya Serikali kwa vitendo.

“Maendeleo ya sayansi na teknolojia yanailazimisha jamii kuwa na ubunifu, na suala hili linaeleweka vyema zaidi kwa vijana. Serikali itaendelea kuweka mipango rafiki, lakini tunahitaji wadau wote kushirikiana nasi kufanikisha hili ili kutuliza kiu ya ajira kwa vijana wetu,” alisema Sangu.

SULUHU YA KIU YA AJIRA

Akizungumzia namna programu hiyo itakavyosaidia vijana, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Benki ya CRDB, Tully Mwambapa, alisema kupitia programu ya IMBEJU, wamejipanga kuchochea ujasiriamali kwa kutoa maarifa, ujuzi, na mitaji wezeshi.

Alibainisha kuwa jukwaa la "Bongo Fursa Show" litazunguka mikoa yote nchini ili kuwafikia vijana walipo, likilenga kuboresha mipango yao ya biashara na kuwaunganisha na fursa za masoko na mitaji kwa ajili ya kupanua biashara changa.

"Tunashirikiana na Serikali kuweka mazingira rafiki ya kukuza biashara. IMBEJU ni jukwaa litakalowaunganisha vijana na fursa za mitaji ili kukuza na kupanua biashara zao, jambo ambalo litaongeza nafasi za ajira kwa vijana wengine," alisema Tully.

MAPINDUZI YA KIDIJITI

Katika kile kinachoonekana kama suluhu ya kudumu ya upatikanaji wa taarifa, chama cha NEDC kimezindua jukwaa la kidijiti la “FURSA HUB”. Jukwaa hili litakuwa kituo kikuu cha mafunzo na taarifa za biashara, likimsaidia kijana aliyepo mkoani kupata ujuzi na fursa za kiuchumi kwa njia ya mtandao.

Mkurugenzi wa Manunuzi wa Benki ya CRDB, Pendason Philemon, aliongeza kuwa kuwekeza kwa vijana ni kuwekeza katika mustakabali wa uchumi wa taifa, akisisitiza kuwa CRDB Bank Foundation imejikita katika kutafsiri sera za kitaifa kuwa fursa halisi zinazogusa maisha ya vijana moja kwa moja.

Ushirikiano huu wa kimkakati kati ya Serikali, Benki ya CRDB, na NEDC unatajwa kuwa nguzo muhimu itakayosaidia vijana wengi kutoitegemea sekta ya umma pekee kwa ajira, bali kuwa wabunifu na wazalishaji wa fursa mpya za kazi kupitia ujasiriamali.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com