Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NEEMA YA KIDIJITALI: SERIKALI YASHUSHA ADA KWA WANABLOGU, TCRA YAZINDUA REDIO YA KISASA 'DSB'


Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma maarufu kama Mwana FA, akizungumza wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Vyombo vya Utangazaji  

****

SERIKALI imetangaza neema ya kihistoria kwa wanablogu, vijana wabunifu, na watoa maudhui mtandaoni nchini kwa kupunguza ada za leseni kwa kiwango kikubwa, hatua inayolenga kuchochea ukuaji wa uchumi wa kidijitali na kurasimisha shughuli za wahabarishaji wa mitandao.

Hatua hiyo imekuja kufuatia utafiti wa kina na mikutano ya kimkakati ya takribani mwaka mzima kati ya mtandao wa Tanzania Bloggers Network (TBN) na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ikielezea vikwazo vya gharama vilivyokuwa vikikwaza uandishi wa habari za kidijitali nchini.


Akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano wa Mwaka wa Watoa Huduma za Utangazaji (ABC 2026) jijini Dodoma leo, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamisi Mwinjuma, amesema ada ya leseni kwa watoa maudhui mtandaoni imeshushwa kutoka Sh500,000 hadi Sh50,000 tu, huku ada ya maombi ikiwa ni Sh10,000 pekee.

Mageuzi hayo pia yamegusa kundi la wakusanyaji wa maudhui (Online Content Aggregators), ambao ada yao imeshushwa kutoka Sh1,000,000 hadi Sh100,000 pekee. Aidha, kundi la "Amateteur" limeanzishwa kwa ajili ya vijana wanaochipukia ili waweze kujitambulisha rasmi na kukuza vipaji vyao bila vikwazo vya kifedha.

Mapinduzi ya Teknolojia ya DSB

Wakati neema hiyo ikitangazwa, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dkt. Jabiri Bakari, ametangaza kuanza kwa teknolojia mpya ya utangazaji wa redio ya kidijitali nchini inayojulikana kama Digital Sound Broadcasting (DSB).

Teknolojia hiyo itaanza kufanya kazi katika mikoa mitano ya majaribio ya Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Arusha, na Mbeya, lengo likiwa ni kuongeza ubora wa sauti na huduma za utangazaji nchini.

"Tumekamilisha maandalizi yote ya kiudhibiti na watoa huduma wa miundombinu wameshapatikana. Hii ni hatua kubwa ya kuendana na mabadiliko ya teknolojia duniani na kuimarisha utangazaji, hususan maeneo ya vijijini," alisema Dkt. Bakari.

Utafiti: Redio Bado ni Kinara

Katika mkutano huo, Injinia Andrew Kisaka wa TCRA amewasilisha matokeo ya utafiti wa hali ya utangazaji kwa mwaka 2025/2026, ukionyesha kuwa redio inaendelea kuwa chanzo kikuu cha habari kwa asilimia 85 ya Watanzania.

 Hata hivyo, utafiti huo umebaini ukuaji mkubwa wa matumizi ya intaneti miongoni mwa vijana, ambapo asilimia 45 hupata habari kupitia mitandao ya kijamii kabla ya kusikiliza redio au kutazama televisheni.

Upande wa televisheni, utafiti unaonyesha asilimia 65 ya watazamaji wanatumia ving'amuzi, huku maudhui ya ndani yakipendwa zaidi kwa asilimia 70. Serikali imewahimiza watoa huduma za kienyeji kuwekeza zaidi kwenye majukwaa ya kidijitali (OTT) ili kukidhi mahitaji ya soko la sasa.

Ulinzi wa Hakimiliki na Mikopo

Ili kuhakikisha wanahabari wa kidijitali wanufaika na kazi zao, Serikali imezielekeza taasisi za COSOTA na TCRA kuandaa mpango wa kulinda hakimiliki na kudhibiti uharamia mtandaoni. Aidha, Serikali imeanza kutoa mikopo ya masharti nafuu kwa watengeneza maudhui kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kisasa vya kufanyia kazi.

Hadi kufikia Desemba 2025, TCRA imetoa jumla ya leseni 707 za utangazaji, zikiwemo 318 za maudhui mtandaoni, jambo linaloashiria kukua kwa uhuru wa habari na demokrasia nchini chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com