Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NATURE TANZANIA YATOA ELIMU YA UHIFADHI KUELEKEA MAADHIMISHO YA SIKU YA WANYAMA DUNIANI JIJINI ARUSHA

Na Bora Mustafa, Arusha.

Kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanyama Duniani, shirika la Nature Tanzania limefika jijini Arusha kwa ajili ya kutoa elimu ya uhifadhi wa wanyama, hususan ndege, ili kupinga vitendo vya uwindaji na imani potofu zinazosababisha baadhi yao kuuawa.

Afisa Mradi Neema Mwaja amesema Maadhimisho hayo yanatarajiwa kufanyika katika Viwanja vya Nane Nane kuanzia Februari 27 mpaka Machi 03 ,2026, Njiro, ambapo shirika hilo linaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kulinda wanyama pori na kuhifadhi mazingira yao.

Kwa mujibu wa shirika hilo, ndege wa mwaka 2026 amepigiwa kura nyingi na kuibuka mshindi ni ndege tausi. Hatua hiyo inalenga kuhamasisha jamii kutambua umuhimu wa ndege huyo katika mfumo wa ikolojia na kuimarisha juhudi za uhifadhi wake.

Afisa Mradi wa Nature Tanzania, Neema Mwaja, amesema shirika hilo ni taasisi isiyo ya kiserikali inayofanya kazi katika mikoa mbalimbali nchini kwa lengo la kulinda  na kuelimisha jamii kuhusu matumizi sahihi ya rasilimali .

Pia amesema bado kuna changamoto ya imani potofu kuhusu baadhi ya ndege, ikiwemo ndege tumbusi, ambapo baadhi ya watu wanaamini kuwa kumuua na kutumia viungo vyake kama dawa kunaweza kuwapa uwezo wa “kuona mbali” au kuwa na mafanikio maishani, kufuatia tabia ya ndege huyo kuona mzoga akiwa umbali mrefu.

Amesema kutokana na hali hiyo, shirika limekuwa likitoa elimu kwa wananchi na hata waganga wa kienyeji ili kuhamasisha matumizi ya mimea tiba badala ya kutumia viungo vya ndege kama jicho au kichwa chake.

 
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuhifadhi miti kwa sababu ndege hutumia miti kama makazi, sehemu ya kuzaliana na chanzo cha chakula kwa ajili ya watoto wao.

Amesema uharibifu wa misitu unaathiri moja kwa moja maisha ya ndege na wanyama wengine, hivyo jamii inapaswa kushiriki kikamilifu katika juhudi za upandaji na utunzaji wa miti.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com