Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DOLA NA MABILIONI: SERIKALI YAFUNGUA MILANGO YA UTAJIRI KWA WASANII NCHINI

 
Usiku wa Februari 14, huku zulia jekundu (Red Carpet) katika ukumbi wa The Super Dome Masaki likiwaka moto kwa nakshi na mitindo, ujumbe mmoja mzito ulitawala anga: Filamu za Tanzania sasa ni biashara ya kimataifa, si mradi wa sinema tu, na vijana lazima kujipamnga kuvuna fursa hizo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, amewataka wasanii nchini kubadili ‘script’ za kazi zao na kuandika hadithi zitakazoshindana duniani na kuleta fedha za kigeni (Dola), akisisitiza kuwa serikali imeshaweka mazingira ya "High Definition" (HD) kwa ajili yao.

Katika kilele cha hotuba yake, Msigwa alibainisha kuwa mpango wa Rais Samia Suluhu Hassan wa kujenga studio ya kisasa ya Shilingi Bilioni 150 ni ishara tosha kuwa safari ya ushindi katika tasnia ya filamu imeanza.

“Tukisimamia ubora na filamu zetu zikafikia viwango vya kimataifa, watengeneza filamu ni mabilionea duniani. Ukifanya kazi kwa mazoea au ‘heya heya’, utaishia kupata milioni mbili, lakini ukizingatia utaalamu, unatafuta mabilioni,” alisema Msigwa huku akishangiliwa na wadau wa tasnia.

Katibu Mkuu hakumung’unya maneno kuhusu ushindi wa wasanii wageni na chipukizi waliojitokeza safari hii. Alieleza kuwa siri ya mafanikio yao ni kwenda shule na kufuata maelekezo ya kitaalamu. 

Alimtaja Profesa Mhando kama mmoja wa wabobezi wanaoandaa maandiko na miongozo ya kitaalamu ili kuwapata wasanii wanaojua misingi ya ubora. “Tusipoandaa wasanii kutekeleza kazi hizi kwa weledi, hata tukiweka miundombinu, itakuwa kazi bure,” alionya.

Kujirudia kwa majina ya washindi kulielezwa kuwa ni matokeo ya majaji wabobezi wanaokagua kazi kitaalamu na si kwa hisia. lengo likiwa ni kuhakikisha TAFFA inakuwa na viwango vinavyotambulika nje ya mipaka, ambapo filamu zinazoshindana zinatakiwa kuwa ni kazi za sanaa (Artistic works) na si miradi ya kutafuta pesa ya haraka.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com