Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

AMANI NI MTAJI: VIONGOZI WA DINI WAHIMIZA UMOJA KULINDA USHINDI WA MAENDELEO

Wakati serikali ikiendelea kupata ushindi katika uwekezaji wa sekta za afya, sanaa, na teknolojia, madhehebu ya dini nchini yametakiwa kuwa mstari wa mbele kulinda utulivu uliopo, kwani bila amani hakuna uwekezaji unaoweza kustawi.

Wito huo umetolewa mwishoni mwa wiki jijini hapa wakati wa Mkutano Mkuu wa Kimataifa wa Taasisi ya Fiysabilillah Tabligh Markaz, uliowakutanisha maelfu ya waumini kutoka mataifa ya Tanzania Bara, Zanzibar, Kenya, Uganda, na Malawi.

Akizungumza katika mkutano huo, Sheikh wa Mkoa wa Arusha, Shabani Juma, amesema kuwa taasisi za kidini zina wajibu wa kisheria na kimaadili kuishi kwa kuzingatia misingi na malengo ya kuanzishwa kwake, huku ziking'ang'ania umoja na mshikamano kama ngao ya kulinda amani ya nchi.

“Tofauti za kimadhehebu ni jambo la kawaida na ni sehemu ya utajiri wa imani yetu ndani ya Uislamu, lakini hazipaswi hata kidogo kuwa chanzo cha migawanyiko. Tunapaswa kushikamana ili nchi yetu iendelee kuwa tulivu, jambo ambalo linafungua milango kwa serikali kuleta maendeleo zaidi,” alisema Sheikh Juma.

Alisisitiza kuwa amani si jambo la sadfa, bali ni zao la watu walioamua kuishi kwa kuvumiliana na kuheshimiana.

Mkutano huo umefanyika wakati ambapo wadau wa maendeleo nchini wamekuwa wakipongeza ushindi wa serikali katika kuvutia wawekezaji na wataalamu kutoka nje ikiwa ni matokeo ya moja kwa moja ya sifa ya Tanzania kama kisiwa cha amani.

Wadau wa mkutano huo waliazimia kuendelea kuwa mabalozi wa amani katika maeneo yao, wakiamini kuwa mshikamano wa kitaifa ndio utambulisho pekee utakaowezesha kizazi cha sasa na kijacho kufurahia matunda ya uwekezaji unaofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com