Na OWM - TAMISEMI, Dodoma
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Selemani Kakoso ameipongeza Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) kwa kujenga miundombinu ya barabara iliyookoa maisha ya wananchi katika maeneo mbalimbali ambayo awali kuharibika kwa miundombinu hiyo kulisababisha vifo vya wananchi.
Mhe. Kakoso amesema hayo leo Februari 11, 2026 wakati wa kikao cha mafunzo kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, yaliyohusu uboreshaji wa Mtandao wa Barabara za Wilaya, Mikakati, Changamoto na Fursa kwa Maendeleo ya Taifa yaliyofanyika katika Ukumbi wa Anne Makinda Bungeni Jijini Dodoma.
Mhe. Kakoso amesema kuwa, katika jimbo lake kuna eneo ambalo TARURA imejenga daraja ambapo kila mwaka wananchi walikuwa wakipoteza maisha kutokana na kukosekana kwa daraja la uhakika, lakini tangu daraja hilo lijengwe hakuna taarifa za vifo tena.
“Katika Jimbo langu kuna sehemu ambayo toka nchi ipate uhuru haijawahi kuwa na barabara lakini TARURA imejenga barabara katika eneo hilo na sasa wananchi wananufaika nayo,” ameeleza Mhe. Kakoso.
Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Florent Kyombo amesema licha ya Serikali kufanya vizuri katika ujenzi wa miundombinu ya barabara katika majiji, ameishauri TARURA kufanya mgao mzuri wa rasilimali fedha ili na maeneo mengine yenye uhitaji yanufaike na ujenzi wa miundombinu hiyo ya barabara.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu -TAMISEMI Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amewahakikishia wajumbe wa kamati hizo kuwa, maoni yote yaliyowasilishwa na wajumbe wa kamati hizo yamepokelewa na yatafanyiwa kazi na wataalam ili kuongeza ufanisi katika ujenzi wa miundombinu ya barabara na hatimaye wananchi kunufaika na miundombinu hiyo.
Katika kukabiliana na majanga, Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Victor Seff amesema kupitia dirisha la majanga (Crisis Management Window) Tanzania imeidhinishiwa mkopo wa nyongeza wa Dola za Kimarekani Milioni 100 kwa ajili ya kurejesha miundombinu iliyoharibiwa na mvua za elnino na kimbunga hidaya cha mwaka 2024, ambapo Dola Milioni 30 ni kwa ajili ya barabara za wilaya na Dola Milioni 70 ni kwa ajili ya barabara za kitaifa.










Social Plugin