Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RAIS SAMIA ADHIHIRISHA UPENDO WAKE KWA KUWAJENGEA ICU WANANCHI HANDENI - PROF. SHEMDOE

Na OWM – TAMISEMI, Handeni

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kujenga jengo la Wagonjwa Mahututi (ICU) katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji Handeni ili kuokoa maisha ya wananchi wa Handeni, kitendo ambacho kinadhirisha upendo wake kwa wananchi hao. 

Prof. Shemdoe amesema hayo leo Februari 13, 2026 katika Viwanja vya Handeni Square, alipopewa fursa ya kuzungumza na wananchi kabla ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba kuzungumza na wananchi hao, mara baada ya Mhe. Waziri Mkuu kuhitimisha ziara yake ya kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo inayotekelezwa Wilayani Handeni. 

“Ndugu zangu wa Handeni tumshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha fedha za ujenzi wa jengo hili la ICU, wengine si rahisi kutambua umuhimu wa jengo hili kwasababu hawajaugua na kulazimika kulazwa ICU, ni jengo muhimu la kuokoa maisha ya mwanadamu,” amesisitiza Prof. Shemdoe.

Kwa kutambua umuhimu wa majengo ya ICU, Prof. Shemdoe amesema  Ofisi ya Rais - TAMISEMI inaendelea kuangalia uwezekano wa kujenga majengo ya ICU Lushoto na Mkinga ili kuboresha huduma za tiba katika maeneo hayo, na kuongeza kuwa ofisi yake inaendelea na jitihada za kuhakikisha hospitali za wilaya ambazo hazina majengo hayo zinapata ili kuokoa maisha ya wananchi.

Kwa upande wake. Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI (Elimu) ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Handeni Mjini Mhe. Reuben Kwagilwa amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha ujenzi wa jengo la Wagonjwa Mahututi, Maabara, Huduma za Dharura na na jengo la kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji Handeni ambayo miundombinu yake ilikuwa chakavu kwani ilijengwa mwaka 1961.
 
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji Handeni, Dkt. Hudi Muradi amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha zilizowezesha kujenga miundombinu katika hospitali hiyo, hivyo amemuahidi Mhe. Rais pamoja na wananchi kuwa, watatoa huduma bora na kuilinda miundombinu hiyo ili  itumike kwa muda mrefu. 

Aidha, kwa niaba ya wakazi wa Handeni Bw. Khalid Hassan Malungula ameishukuru Serikali kwa kujenga jengo la ICU ambalo limeboresha utoaji wa huduma kwa wagonjwa mahututi, na kueleza kuwa kabla ya ujenzi wa jengo hilo wagonjwa wa kawaida na mahututi walikuwa wakihudumiwa  pamoja.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com