
Binti mmoja mkazi wa Arusha, Jennifer Paschal, anaendelea kuomba msaada wa kifedha kutoka kwa Watanzania wenye mapenzi mema baada ya figo zake zote mbili kufeli, hali iliyomlazimu kutegemea huduma ya dialysis ili kuendelea kuishi.
Akiwa katika kipindi cha kusubiri msaada huo, Jennifer alipata nafuu ya muda baada ya taasisi moja kujitolea kumlipia gharama za dialysis kwa kipindi cha miezi mitatu bila malipo. Hata hivyo, muda wa msaada huo unatarajiwa kuhitimishwa mwezi huu wa Machi, jambo linalozua hofu mpya kuhusu mustakabali wa matibabu yake.
Kwa mujibu wa taarifa na vielelezo vya hospitali alivyoviwasilisha, fedha alizokusanya hapo awali zilitumika kugharamia matibabu ya dharura baada ya mshipa (vein) aliokuwa akitumia wakati wa dialysis kupata hitilafu. Upasuaji wa kurekebisha tatizo hilo uligharimu zaidi ya shilingi milioni tatu, hali iliyosababisha fedha nyingi kuishia kwenye matibabu hayo ya haraka.
Kwa sasa, Jennifer hana uwezo wa kifedha wa kuendelea na huduma ya dialysis mara tu msaada wa taasisi utakapokoma. Madaktari wake wamemshauri kuwa suluhisho la kudumu ni kufanyiwa upandikizaji wa figo. Tayari mama yake mzazi ameonesha utayari wa kuwa mtoaji wa figo, lakini zoezi zima la upasuaji na matibabu linahitaji jumla ya shilingi milioni 45,000,000/-.
Kupitia ujumbe wake, Jennifer anaomba msaada kutoka kwa Watanzania, viongozi wa serikali, taasisi za umma na binafsi, pamoja na wadau wote wa afya ili kufanikisha upasuaji huo na kuokoa maisha yake.
Familia yake imesisitiza kuwa kila mchango, mkubwa au mdogo, utakuwa sehemu ya matumaini mapya na hatua muhimu kuelekea kupona kwa binti huyo.
Kwa yeyote mwenye kuguswa na hali hiyo, anaweza kutuma mchango kupitia namba 0740 540 489, jina la usajili ni Jennifer Paskali Jorojick.
“Kila mchango wako ni uhai wangu,” anasisitiza Jennifer huku akiendelea kupambana kwa matumaini ya kuanza ukurasa mpya wa maisha yake.
Social Plugin