
Mbunge wa Jimbo la Kahama Mjini, Mhe. Benjamin Ngayiwa, ameiomba Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) kuharakisha mchakato wa kumpata mkandarasi mpya kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa barabara ambazo kazi zake zimesimama kufuatia Serikali kuvunja mkataba na mkandarasi wa awali, ili kuondoa adha wanayopata wananchi.
Ngayiwa ametoa kauli hiyo Februari 24, 2026, wakati akichangia hoja katika kikao cha tathmini ya utekelezaji wa miradi ya barabara cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Shinyanga , kilichofanyika mkoani humo.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kupatikana kwa mkandarasi mwenye sifa na vigezo vinavyostahili, atakayehakikisha mradi huo unakamilika kwa viwango vinavyotakiwa na ndani ya muda uliopangwa.
Katika hatua nyingine, Mbunge huyo aliishauri TARURA kuandaa mpango mkakati wa kujenga barabara zenye viwango na ubora wa kudumu kwa muda mrefu, ili kupunguza changamoto ya kufanya matengenezo ya mara kwa mara kila mwaka.

Social Plugin