Uanzishwaji wa Jukwaa la Vijana Tanzania (Youth Platform Tanzania) umeleta mwangaza mpya na matumaini kwa maelfu ya vijana nchini.Tofauti na mifumo ya kizamani, Jukwaa la Vijana Tanzania limejikita katika mambo makuu matatu: Kusikiliza, Kuunganisha, na Kutatua.
Kupitia jukwaa hili, vijana kutoka sekta mbalimbali—ikiwemo wajasiriamali, wahitimu wa vyuo vikuu, na wasanii—wanapata nafasi ya kuwasilisha changamoto zao moja kwa moja kwa Waziri mwenye dhamana bila urasimu.
Watu waliohojiwa wanasema kuwa jukwaa hilo linawezesha vijana kupata majibu ya hoja zao kwa kasi, kwani mifumo inayozungumzwa na wapinzani wa jukwaa hilo huchelewesha majibu.Wadau wengi wa maendeleo wanasema jukwaa limeanzishwa wakati sahihi kwani "vijana wanahitaji majibu sasa, si kesho."
Ngome ya Vijana ya chama cha ACT Wazalendo imejitokeza kupinga jukwaa hilo, ikidai kuwa halina msingi wa kisheria na badala yake serikali ingejielekeza kwenye Baraza la Taifa la Vijana (BVT).
Lakini wachambuzi wa masuala ya kijamii na vijana wenyewe wamehoji uzito wa hoja hiyo ya ACT. Katika karne hii ya kasi ya digitali na mabadiliko ya kiuchumi, vijana hawawezi kusubiri mchakato mrefu wa kisheria wa kuunda mabaraza wakati matatizo yao yanahitaji utatuzi wa papo hapo.
"Kuhubiri habari za sheria wakati kijana hana ajira leo ni kama kumpa kitabu cha sheria mtu mwenye njaa. Jukwaa hili ni hatua ya vitendo (Action-oriented platform) ambayo inashughulika na mahitaji ya sasa hivi," alisema mmoja wa vijana waliokuwepo kwenye uzinduzi huo.
Nje ya jiji la Dar es Salaam, vijana wameonyesha kiu ya kutaka kunufaika na jukwaa hili. Hamisi Mtwale, kijana mjasiriamali kutoka Mwanza, anasema: "Sisi huku mikoani hatuhitaji siasa za kisheria, tunahitaji fursa. Waziri anapofungua milango ya kumsikiliza kijana mmoja mmoja, anatuondolea kuta ambazo zilikuwepo kwa miaka mingi."
Naye Mariam Juma, mkulima kijana kutoka Morogoro, aliongeza kuwa jukwaa hili ni fursa ya kipekee kwa vijana wa vijijini kufikisha kilio chao cha mitaji na masoko bila kusubiri mikutano mikubwa ya mabaraza.
Waziri mwenye dhamana na vijana,Joel Nanauka amekuwa akisisitiza kuwa ofisi yake iko wazi na imejielekeza zaidi kwenye kutumia teknolojia na mawasiliano ya moja kwa moja. Hii ni kasi inayotofautiana na hoja za "kikaratasi" zinazotolewa na upinzani ambazo zinaonekana kuchelewesha utekelezaji. Serikali inaonekana kutaka kuunganisha vijana wote bila kujali itikadi zao, ili kwa pamoja "Tujenge Tanzania Yetu."
Social Plugin