Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAKILI MUTABUZI: TUVUKE VIKWAZO VYA OKTOBA 29, AMANI NDIO KILA KITU

WAKILI wa kujitegemea, Mwesigwa Mutabuzi, ametoa wito wa kitaifa kwa Watanzania kujitambua na kuthamini amani kama tunu kuu ya taifa, huku akionya kuwa kubaki na vinyongo kutokana na matukio ya vurugu za tarehe 29 Oktoba ni hatari kwa usalama wa nchi na maendeleo ya mtu mmoja mmoja.

Wakili Mutabuzi, ambaye hivi karibuni gari lake lilichomwa moto wakati wa vurugu hizo, amesema ni wakati wa "kuganga yajayo" na kuacha chuki ambazo zinaweza kuligawa taifa na kusababisha madhara makubwa zaidi ya yale yaliyokwisha kutokea.

Wito kwa Wanasheria na Viongozi wa Dini

Akizungumza ofisini kwake jijini Dar es Salaam, amewataka wanasheria, wanaharakati, viongozi wa dini na wadau wa maendeleo kutumia taaluma na ushawishi wao kudumisha uzalendo na mshikamano. Amesema taaluma zisitumike kuchochea migawanyiko, bali ziwe nyenzo ya kutatua changamoto za kijamii kwa kufuata misingi ya sheria na mazungumzo.

Amesisitiza kuwa wanaharakati wana wajibu wa kuelimisha jamii kwa kutumia lugha ya staha na hoja zenye kujenga, badala ya kuchochea vitendo vya uhalifu ambavyo mwisho wa siku huacha makovu katika mioyo ya wananchi.

Pongezi kwa Jeshi la Polisi

Wakili huyo amepongeza juhudi za Jeshi la Polisi kwa namna lilivyokabiliana na uchochezi uliokuwa unahatarisha usalama wa raia. Ameliomba jeshi hilo kuendelea na uchunguzi wa matukio hayo ya uhalifu na vurugu huku akiwasihi wananchi kuwa watulivu na kuepuka kauli zinazoweza kuamsha upya vinyongo vya kisiasa.

Ingawa baadhi ya maoni ya wadau (mitandaoni) yanashauri kuwepo kwa suluhu za kudumu kama maboresho ya Katiba ili kumaliza kiini cha migogoro, Mutabuzi anaamini kuwa hatua ya kwanza ni utulivu wa nafsi na kuamua kwa dhati kulinda amani iliyopo sasa wakati mchakato wa kisheria na kijamii ukiendelea. 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com