Tunapoendelea na mwaka mpya wa 2026, rai imetolewa kwa wazazi na walezi kutokaimisha jukumu la malezi ya watoto wao kwa watu wengine na badala yake watenge muda wa kulea na kukuza watoto wao katika misingi na tamaduni zinazokubalika ili kuondokana na kadhia kadhaa za uduni wa malezi ikiwemo tabia ovu na tamaduni za kigeni ambazo zimekuwa zikiathiri jamii na Taifa kwa ujumla.
Rai hiyo imetolewa na Bi. Grace Kafulama, Mkazi wa Kigoma, wakati akizungumza nasi kuhusu umuhimu wa malezi ya wazazi kwa watoto kama msingi wa amani na usalama ndani ya jamii na Taifa kwa ujumla, akisema masuala hayo huanza ndani ya familia zinazowajibika vyema katika malezi ya watoto hao.
Bi. Kafulama amesisitiza kuwa malezi kwa watoto si kugharamia mahitaji ya mtoto peke yake, bali ni pamoja na kuzungumza na watoto, kuwafundisha na kuwaelekeza kuhusiana na masuala mema, akisema jukumu hilo ni la kila mzazi na mlezi kama ilivyokuwa zamani.
"Kwasasa tupo kwenye jamii ambayo tunashuhudia baadhi ya watoto wakifanya mambo ya ajabu na kwasababu si mtoto wako unaamua kumuacha kwamba atajua mwenyewe. Tusimame kutimiza wajibu wetu, wewe mzazi ni balozi wa kwanza wa kukemea, kuonya na kuelimisha juu ya matendo mema na kuwatengenezea mazingira bora ya kesho, hakuna Waziri ama serikali itakayomtengeneza mtoto kama sisi jamii na wazazi hatutawajibika vyema." Amesema Bi. Kafulama.
Katika hatua nyingine, Bi. Kafulama amezungumzia pia chanzi cha vurugu za wakati na baada ya uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, akisema kwa kiasi kikubwa matukio yale yamesababishwa na kudhorota kwa malezi ya Vijana nchini, akisema ikiwa kila mzazi atawajibika vyema ni aghalabu kwa wananchi kushiriki katika kuharibu amani ya Tanzania.

Social Plugin