Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAFUNGUA MLANGO WA KITAIFA KWA BIASHARA YA SENENE





Na Josephine Manase,Dodoma.

Baada ya miaka mingi biashara ya senene kuonekana kama shughuli ya msimu na ya kienyeji isiyopewa kipaumbele cha kitaifa, Serikali sasa imeanza hatua za makusudi za kuifungua na kuikuza ili iwe chanzo rasmi cha ajira, kipato na fursa za biashara ndani na nje ya nchi.

Kauli hiyo imetolewa bungeni leo 30 Januari, 2026 na Naziri wa Viwanda na Biashara Judith Kapinga wakati akijibu la Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini, Johnston Mutasigwa, aliyehoji mpango wa Serikali wa kuwapatia wauza senene masoko ya uhakika pamoja na vifaa bora vya kutegea zao hilo.

Akijibu, Waziri amesema Serikali inaendelea kutafuta na kufungua masoko ya uhakika kwa bidhaa za senene, ikiwemo kuwaunganisha wafanyabiashara wa senene na masoko ya miji mikubwa nchini.

Amesema hatua hiyo inalenga kupanua wigo wa zao hilo kutoka biashara ya eneo moja kwenda bidhaa ya kitaifa.

Ameongeza kuwa wauza senene wanashirikishwa pia katika maonesho ya biashara ya kitaifa na kikanda, sambamba na jitihada za kuitangaza senene kama bidhaa ya kipekee ya Kanda ya Ziwa, yenye uwezo wa kuingia katika masoko mapana ya Afrika Mashariki na kwingineko duniani.

Katika kueleza mwelekeo huo mpya, Naibu Waziri amesema Serikali inatambua fursa ya kiuchumi iliyopo katika zao hilo, na kwamba kulipa thamani ni sehemu ya mkakati wa kukuza viwanda vidogo, kuendeleza uchumi wa wananchi na kuongeza wigo wa bidhaa za asili zinazochangia pato la taifa.

Amesema Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO), kwa kushirikiana na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) pamoja na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), imeendelea kufanya tafiti mbalimbali zinazolenga kuboresha na kuendeleza biashara ya senene, hususan katika Mkoa wa Kagera ambako zao hilo linapatikana kwa wingi.

“Mpaka sasa, teknolojia rahisi ya mfano (prototype) inayosaidia katika uvunaji wa senene imebuniwa na kutengenezwa, hatua itakayosaidia kuongeza ufanisi, usalama na tija katika uvunaji wa senene,” amesema Naibu Waziri.

Hatua hiyo ya Serikali inaashiria mabadiliko ya sera na mtazamo kuhusu biashara ya senene, kutoka kuwa shughuli isiyo rasmi hadi kuwa bidhaa yenye thamani ya kitaifa na kikanda, inayoweza kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya viwanda na uchumi .

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com