Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MTEGO WA KISAIKOLOJIA: JINSI WACHOCHEZI WA MTANDAONI WANAVYOTUMIA HISIA ZAKO KAMA SILAHA


Katika ulimwengu wa kidijitali, vijana ndio kundi lenye nguvu kubwa zaidi, lakini pia ndilo linalolengwa zaidi na wachochezi wa mtandaoni. Wachochezi hawa, mara nyingi wakiwa wamejificha nyuma ya vioo vya simu zao katika mazingira salama, hutumia mbinu za kisaikolojia ili kuwafanya vijana waingie mitaani kufanya vurugu. Ni muhimu kuijua mitego hii ili usitumike kama daraja la maafa huku wengine wakivuna faida wakati wewe ukibaki na makovu ya maisha.

Mtego wa kwanza ni kutumia hasira na uchezaji wa hisia ambapo wachochezi hawa hawaji na hoja za kimantiki au suluhisho la kisayansi, bali huja na lugha ya kuudhi, matusi, na kashfa. Lengo lao kuu ni kukufanya uwe na hasira ya ghafla kiasi cha kushindwa kutumia busara. Binadamu anapokuwa na hasira kali, sehemu ya ubongo inayofanya maamuzi ya busara hupungua kasi, na hapo ndipo mchochezi anapoweza kukuamrisha kufanya lolote, ikiwemo kuvunja sheria. Ni vyema kukumbuka kuwa mtu anayekutukana au kukuchochea uwe na hasira, haheshimu akili yako bali anaitumia kama chombo cha mashambulizi.

Mbinu nyingine ya kisaikolojia ni kuonyesha maisha ya "bata" dhidi ya maisha ya "shida" ili kujitengenezea taswira ya ushujaa huku wakiishi maisha ya kifahari. Huenda ukaona picha zao wakiwa kwenye migahawa mikubwa, wakisafiri nchi za nje, na watoto wao wakiwa shule za gharama. Wanachokifanya ni kukupa wewe picha ya ushujaa wa mtandaoni ili uingie mtaani kupambana na vyombo vya dola, wakati wao wanarekodi video wakiwa wanakunywa vinywaji baridi. Wanatumia hali yako ya utafutaji kama fimbo ya kukupondea, huku wao wakiwa hawako tayari kupata hata mkwaruzo mmoja kwa ajili ya kile wanachokihubiri.

Vilevile, wachochezi hupenda kutengeneza mazingira ya kuwa na adui wa kufikirika kwa kuaminisha watu kuwa kila tatizo lina mhusika mmoja wa kulaumiwa na njia pekee ya kumaliza tatizo hilo ni vurugu. Wanatengeneza mazingira ya mipasuko ya kijamii yanayofuta uwezekano wa mazungumzo na maridhiano. Vijana wengi huingia kwenye mtego huu na kuanza kuona ndugu zao, majirani, au askari kama maadui, badala ya kuona mifumo ambayo inapaswa kurekebishwa kwa hekima, sheria, na taratibu zilizopo bila kumwaga damu.

Kwenye mitandao ya kijamii, wachochezi hutengeneza hali ya shinikizo la makundi na hofu ya kutengwa ili kumfanya kijana ajihisi kuwa ukiwa mshabiki wao lazima uandamane. Hali hii inamfanya kijana aogope kuonekana muoga au msaliti kwa wenzake wa mtandaoni. Wachochezi hutumia saikolojia ya kundi kuwafanya vijana wajihisi kuwa sehemu ya harakati kubwa, kumbe ni harakati zinazolenga kuharibu mustakabali wa maisha yao binafsi huku wahusika wakuu wakibaki salama kwenye kuta za nyumba zao ughaibuni.

Mitego hii huambatana na ahadi za uongo na matumaini hewa kwa kudai kuwa vurugu zikiisha, kila kitu kitakuwa sawa kesho yake. Huu ni uongo wa kisaikolojia kwani historia inaonyesha kuwa nchi yoyote iliyoingia kwenye vurugu za kilele, ilichukua miongo kadhaa kurudi ilivyokuwa.

Gharama ya maisha hupanda, ajira hupotea, na wawekezaji hukimbia. Wachochezi hawaelezi kuhusu vifo, vilema, na rekodi za uhalifu zitakazokufuata maisha yako yote. Ukomavu ni kutambua kuwa unaweza kukosoa na kudai haki yako bila kufuata maelekezo ya mtu anayekula bata ughaibuni. Kulinda amani si uoga, ni akili na ushujaa wa kweli unaolinda uhai wa leo na matumaini ya kesho.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com