
Tofauti na siku za karibuni ambapo sauti za mihemko ziliweza kuyumbisha fikra za wengi, leo hii Watanzania wameamua kuweka mbele maslahi ya taifa kwa kukataa katakata kufuata wito wa vurugu unaotolewa na watu wanaoishi maisha ya anasa ughaibuni wakitaka kuyaendeleza kupitia maafa ya Tanzania.
Mabadiliko haya yanathibitisha kuwa wananchi wametambua mtego wa "wanaharakati wa kashfa" ambao huchochea machafuko kupitia mitandao huku wao wenyewe wakiwa wamelindwa na amani ya mataifa mengine, jambo linaloacha mzigo wa madhara kwa vijana na raia wa kawaida nchini.
Kushindwa kwa juhudi za watu kama Mange Kimambi na wengineo katika kuhamasisha maandamano ya vurugu ni kielelezo tosha kuwa mbinu za kupandikiza hofu na chuki hazina tena soko nchini Tanzania.
Licha ya kutumia nguvu kubwa ya mitandao na lugha za kashfa, mwitikio wa wananchi umekuwa mdogo kwa sababu watu sasa wanahoji vyanzo vya habari na nia ya mtoa habari. Badala ya kufuata miongozo ya "mahakama za mitandaoni" zinazoendeshwa kwa maslahi ya wachache, Watanzania wamechagua kuamini mifumo rasmi ya ndani ya nchi na njia za maridhiano ambazo zimekuwa zikihimizwa na viongozi wa dini na Serikali kwa ujumla.
Viongozi wa dini wamekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha ukuta huu wa amani kwa kutoa elimu kwa waumini wao kuhusu madhara ya vurugu, wakisisitiza kuwa amani ndiyo msingi pekee wa uchumi na maisha bora.
Wito wao kwa vijana umekuwa ni kutafakari kwa kina kabla ya kujiingiza katika matendo yanayoweza kuharibu mustakabali wa maisha yao, kwani historia inaonyesha kuwa machafuko huacha majeraha ya kudumu huku wahamasishaji wakibaki salama. Hali hii imewafanya vijana wengi kuhamisha nguvu zao kutoka kwenye kufuatilia udaku wa kisiasa usio na tija na badala yake kujikita katika kutumia ubunifu wao kutafuta fursa za kiuchumi zinazolindwa na utulivu wa nchi.
Mazingira ya sasa ya kisiasa yanayotoa nafasi kwa maridhiano na mijadala ya kistaarabu yameziba kabisa mianya ya watu wanaotegemea migogoro ili kupata umaarufu.
Jamii imejenga utamaduni mpya wa kuthamini staha na heshima, ikiamini kuwa mabadiliko ya kweli yanapatikana kupitia hoja na suluhisho mbadala badala ya matusi na vurugu. Hii ni ishara kuwa umoja wa kitaifa ni imara zaidi kuliko jitihada za mtu mmoja mmoja za kutaka kuugawa umma, na kwamba uwekezaji wa wafadhili wa machafuko umegonga mwamba mbele ya busara ya Watanzania ambao wameamua kulinda nchi yao kwa gharama yoyote.
Social Plugin