
Katika kipindi ambacho jamii inakabiliwa na changamoto mbalimbali za kimaadili na kimfumo, somo la kale kutoka Kitabu cha Hesabu Sura ya 16 limeibuka kuwa dira muhimu kwa Watanzania. Uchambuzi wa tukio la kihistoria la uasi wa Kora, Dathani, na Abiramu unatoa onyo kali: Kukataa mamlaka zilizopo si tu kukiuka utaratibu wa nchi, bali ni kualika hukumu ya kimungu na maangamizi.
Kitabu cha Hesabu kinaelezea kwa kina jinsi Kora na wenzake walivyojitokeza kupinga uongozi wa Musa na Haruni. Kwa nje, walionekana kana kwamba wanatetea haki na usawa wa jamii, wakidai kuwa kila mtu ni mtakatifu. Hata hivyo, maandiko yanabainisha kuwa ndani yao kulikuwa na sumu ya kiburi na kiu ya madaraka yasiyo ya halali.
"Uasi huu haukuwa tu dhidi ya binadamu, ulikuwa ni uasi dhidi ya 'God’s Order' (Utaratibu wa Mungu). Mungu ni Mungu wa mpangilio, na anapoweka mamlaka, anategemea nidhamu na utii ili kulinda amani ya wengi," anasema mchambuzi wa maandiko.
Moja ya mambo ya kusikitisha katika simulizi hiyo ni pale Musa alipojaribu kuwaita wapinzani wake (Dathani na Abiramu) ili wazungumze kwenye meza moja ya maridhiano. Kwa dharau, walijibu: "Hatuji!" Msimamo huu wa kukataa mazungumzo na kudharau mamlaka ndio uliopasua mlango wa hukumu. Matokeo yake, ardhi ilipasuka na kuwameza wote waliohusika na uasi huo.
Hii ni fundisho kwa Watanzania wa leo; kwamba kukaa kwenye meza ya mazungumzo na kukiri mamlaka si udhaifu, bali ni hekima ya kiroho inayookoa taifa dhidi ya machafuko.
Ili taifa liendelee, ni lazima kuwe na msingi wa kuheshimiana kati ya viongozi na wananchi: Kukiri mamlaka kunajenga nidhamu na kuzuia "hukumu ya pamoja" inayoweza kuikumba jamii pale uasi unapotawala. Ni lazima kutofautisha kati ya kutoa maoni kwa staha na kufanya uasi kwa nia ya kubomoa. Hayo yanatokana na ukweli kuwa Mfumo wa Mungu unamtaka kiongozi kuwa na moyo kama wa Musa—moyo wa unyenyekevu na utayari wa kusikiliza malalamiko ya watu kabla hayajazaa chuki.
Ukisoma kitabu hicho unang'amua kwamba amani, uwajibikaji, na haki haviwezi kupatikana kupitia mivutano na uasi. Badala yake, vinapatikana pale kila mmoja anapokubali mfumo sahihi uliowekwa na Mungu na sheria za nchi.
"Tunahitaji umoja zaidi ya hapo awali. Unapokataa mamlaka, unachallenge msingi wa utulivu wa taifa. Hukumu ya uasi si lazima iwe ardhi kupasuka, inaweza kuwa kupotea kwa amani, kusimama kwa maendeleo, na kuvunjika kwa misingi ya kijamii," anaongeza mchambuzi huyo.
Watanzania wanahimizwa kuachana na kiburi cha moyoni kinachochochea uasi. Kukiri mamlaka ni ukomavu. Ni ujasiri wa kutambua kuwa sote tunahitajiana chini ya mwavuli mmoja wa uongozi ili kufikia nchi ya ahadi. Tuwe na hekima, tuepuke uasi, na tuchague meza ya mazungumzo kwa ajili ya mustakabali wa taifa letu. Kwa kufanya hivyo, tunaepuka laana ya maangamizi na kuvuta baraka za Mungu juu ya nchi yetu.
"Hekima ya kweli ni kujua kuwa uasi una mwisho wa mauti, lakini utii na maridhiano huleta uzima."
Social Plugin