Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BANDARI ZETU ZINA UWEZO WA KUHUDUMIA MELI KUBWA NA ZA KISASA- MSIGWA



Serikali imeonesha kuridhishwa na ufanisi mkubwa pamoja na kurejea kuaminika kwa bandari ya Dar Es Salaam, akisema kwasasa Meli kubwa zimekuwa zikisimama katika bandari hiyo baada ya uwekezaji wa kuongeza Kina cha bandari hiyo, suala lenye kuwezesha Tanzania kuweza kupokea Meli zenye hadi ukubwa wa Mita 305.

Kulingana na Msemaji Mkuu wa serikali Bw. Gerson Msigwa amesema mafanikio hayo makubwa yanatokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na hivyo kuweza kupunguza gharama za usafirishaji kwa wafanyabiashara wenye mizigo mikubwa ama mingi, suala ambalo lililazimu hapo awali kusafirishwa kwa awamu kutokana na Bandari kukosa uwezo wa kuhudumia meli kubwa.

"Nipo hapa na nyuma yangu mnaona kuna meli ya Galaxy S yenye uwezo wa kubeba magari zaidi ya 6,000 kuna nyingine pia hapa imeleta ngano ikiwa na uwezo wa kubeba tani 60,000 kwa wakati mmoja. Huko nyuma meli hizi zisingeweza kuja hapa kwani gati zetu zilikuwa fupi kuweza kuhimili ukubwa wa meli hizi."

"Kazi hii kubwa iliyofanyika na serikali yetu inatuwezesha sasa kupokea meli ndefu za hadi Mita 305 na hivyo kutuwezesha kupokea meli kubwa nchini na kwa wafanyabiashara, unapokuwa na Bandari za namna hii unasaidia katika uchumi kwani sasa tumepunguza gharama za usafirishaji wa bidhaa mbalimbali." Amesema Bw. Msigwa.

Awali mnamo Disemba 2025, Wizara ya uchukuzi iliripoti pia kwamba bandari ya Dar Es Salaam imevunja rekodi ya kupokea Meli kubwa zaidi ya makasha ya MSC Stella yenye urefu wa Mita 304.40, kutoka bandari ya Jebel Ali Dubai, suala ambalo liliongeza heshima, imani na hadhi ya Bandari za Tanzania Kimataifa pamoja na kuonesha kuimarika kwa uwezo wa bandari katika kuhudumia meli za kisasa na za viwango vya Kimataifa.







Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com