Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

AJIRA ZA WAZAWA MIGODINI ZAONGEZEKA, WAFIKIA ASILIMIA 97



Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Hatua za Serikali kuimarisha ushiriki wa Watanzania katika Sekta ya Madini zimeanza kuleta matokeo chanya, baada ya ajira za wazawa katika miradi ya uchimbaji madini kufikia asilimia 97, hali inayodhihirisha mabadiliko makubwa katika umiliki wa fursa za ajira na uchumi wa rasilimali kwa wananchi.

Takwimu zinaonesha kuwa ajira kwa Watanzania migodini zimeongezeka kutoka ajira 6,668 sawa na asilimia 95 mwaka 2018 hadi kufikia ajira 18,853 kati ya ajira 19,356 ifikapo Desemba 2024, sawa na asilimia 97 ya ajira zote katika sekta hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 5, 2026 jijini Dodoma, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema mafanikio hayo yametokana na utekelezaji thabiti wa sera, sheria na kanuni za ushirikishwaji wa Watanzania (Local Content), zinazolenga kuhakikisha rasilimali madini zinawanufaisha wananchi moja kwa moja kupitia ajira na fursa za kiuchumi.

Amesema Serikali imefanya marekebisho ya Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania za mwaka 2018, ambapo kupitia Kanuni ya 13A, Wizara ya Madini itakuwa ikitangaza mara kwa mara orodha ya bidhaa na huduma zitakazotakiwa kutolewa na kampuni za Kitanzania zinazomilikiwa kwa asilimia 100 na Watanzania.

Waziri Mavunde amesema katika hatua ya awali, Tume ya Madini ilitangaza tarehe 14 Novemba, 2025 orodha ya bidhaa na huduma hizo, hatua inayolenga kupanua wigo wa ajira, kuongeza ushiriki wa wazawa na kukuza uwezo wa kampuni za ndani kushiriki kikamilifu katika miradi ya madini.

“Nitumie fursa hii kuwasisitiza Watanzania kuendelea kujijengea utaalamu unaohitajika katika shughuli za madini, ili waweze kushindana na kustahili fursa za ajira migodini pamoja na utoaji wa huduma katika miradi hiyo,” amesema Mavunde.

Aidha, amewataka watoa huduma kuzingatia viwango na ubora unaotakiwa ili kuendelea kuaminika, huku akisisitiza kuwa wawekezaji wote wanapaswa kuzingatia Sheria ya Madini, Sura ya 123, pamoja na utekelezaji wa Kanuni za Local Content. Watanzania pia wamehimizwa kuchangamkia fursa zilizopo katika sekta hiyo kama njia ya kukabiliana na changamoto ya ajira na kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Ameeleza kuwa Serikali imeweka utaratibu wa kisheria wa kuhakikisha nafasi zilizokuwa zikishikiliwa na wataalamu wa kigeni zinarithishwa kwa Watanzania, hatua inayolenga kujenga uwezo wa kitaaluma na kuongeza idadi ya wazawa katika nafasi za juu za uongozi kwenye migodi ya kati na mikubwa.

Akitolea mfano, Waziri Mavunde amesema Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, unaomilikiwa na Kampuni ya Twiga Minerals Corporation (Barrick Gold), kwa sasa nafasi zote za juu za uongozi zinashikiliwa na Watanzania.

Katika upande wa mapato ya Serikali, amesema mageuzi hayo yamechangia ongezeko kubwa la makusanyo kutoka Sekta ya Madini, yakipanda kutoka Shilingi bilioni 526.722 mwaka 2020/2021 hadi kufikia Shilingi trilioni 1.071 mwaka 2024/2025.

Kwa mwaka wa fedha 2025/2026, Wizara ya Madini imepangiwa kukusanya Shilingi trilioni 1.2, ambapo hadi Desemba 31, 2025, jumla ya Shilingi bilioni 653.139 zilikuwa tayari zimekusanywa, sawa na asilimia 108.86 ya lengo la miezi sita ya kwanza ya mwaka wa fedha.

Katika kuhakikisha Watanzania wananufaika zaidi na ajira na fursa za kiuchumi, Mavunde amesema Wizara kupitia Tume ya Madini imeimarisha usimamizi wa manunuzi migodini kwa kutoa kipaumbele kwa kampuni za Kitanzania, hatua iliyoongeza thamani ya manunuzi ya bidhaa na huduma kutoka Shilingi trilioni 1.85 mwaka 2018 hadi kufikia Shilingi trilioni 4.41 mwaka 2024, sawa na asilimia 88 ya manunuzi yote.

Ameongeza kuwa Serikali imeendelea kuhamasisha ujenzi wa viwanda vinavyozalisha bidhaa zinazohitajika kwa wingi migodini, hali iliyochochea uwekezaji wa kampuni za Kitanzania zikiwemo Rock Solutions Limited, Max Steel na East Africa Conveyors Supplies Limited, ambazo zimejenga viwanda kwa kushirikiana na wazalishaji wa kimataifa, huku bidhaa zikisambazwa ndani na nje ya nchi.

Pamoja na hatua hizo, Waziri Mavunde amesema Tume ya Madini imeanzisha Majukwaa ya Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini yanayofanyika kila mwaka, yakihusisha wamiliki wa leseni, watoa huduma, wasambazaji wa bidhaa migodini, taasisi za Serikali pamoja na Wizara ya Madini na taasisi zake.

Amesema hadi sasa majukwaa manne yamefanyika kwa mafanikio makubwa, yakilenga kuimarisha utekelezaji wa Local Content na kuhakikisha Sekta ya Madini inaendelea kutoa manufaa mapana kwa Watanzania na Taifa kwa ujumla.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com