Shirika la Masoko ya Kariakoo limetoa zawadi za Sikukuu za Krismasi na mwaka mpya kwa watumishi wake ikiwa ni sehemu ya motisha kwa utendaji kazi wao mzuri waliouoneshakwa mwaka 2025 ambao umechangia shirika hilo kutoa huduma kwa wateja wake kwa ufanisi, weledi na kwa wakati.
Akikabidhi zawadi hizo, Meneja Mkuu wa Shirika hilo, CPA. Ashraph Abdulkarim amesema utendaji kazi wa watumishi wa shirika hilo umesaidia kuwapangia wafanyabishara wa zamani takribani 1520 maeneo ya biashara, kufanya uchambuzi na kuwapangia maeneo ya biashara wateja wapya 351, kuingiza mikataba ya wateja kwenye mfumo wa TAUSI na pia kushughulikia malalamiko na changamoto za wafanyabiasha kwa wakati na weledi.
Aidha, CPA. Abdulkarim amewahimiza watumishi hao kuendelea kufanya kazi kwa bidii, weledi na kufuata sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza utumishi ili kuendelea kuchochea mabadiliko ya utendaji kazi wa shirika hilo na kutokubweteka.
CPA. Abdulkarim amebainisha kuwa soko la Kriakoo ambalo linasimamiwa na shirika hilo linapaswa kuendeshwa kisasa na kulifanya liwe soko linalotoa huduma anuai badala ya kuwa soko la mazao ya kilimo pekee kama ilikuwa hapo awali.
“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inataka kuona matokeo, hivyo kila mmoja katika nafasi yake anapaswa kuona ni kwa namna gani anaweza kuleta matokeo chanya katika kutoa huduma na kufanya shirika hilo kujiendesha kibiashara zaidi” ameongeza CPA. Abdulkarim
CPA. Abdulkarim ameongeza kuwa ili kuhakikisha watumishi wanafanya kazi vizuri, shirika litaendelea kusimamia na kutoa stahiki zao kwa wakati, huku ikiweka mkazo katika kuwajengea uwezo wa mara kwa mara ili kuendana na mabadiliko yanayojitokeza mara kwa mara duniani.




Social Plugin