Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) David Misime amesema hali ya usalama ni shwari kote nchini Tanzania na shughuli za kiuchumi na kijamii zinaendelea kama kawaida nchi nzima baada ya mapumziko ya sherehe za sikukuu ya Uhuru wa Tanzania bara jana Jumanne Disemba 09, 2025.
Kulingana na taarifa yake kwa Vyombo vya habari, Jeshi la Polisi kwa ushirikiano na Vyombo vingine vya ulinzi na usalama vitaendelea kushirikiana na wananchi kuhakikisha amani na usalama unaendelea kuimarika nchini ili hata wale wachache wenye hofu waweze kutoka na kuendelea na shughuli zao za kila siku za kujitafutia riziki na kupata huduma za kijamii wanazo hitaji.
"Aidha tunawashukuru na kuwapongeza wananchi wote kwa nafasi zao kwa namna wanavyoendelea kuwakataa na kuwapuuza wale wanaohamasisha na kuchochea vurugu na ukiukwaji wa Sheria za nchi kupitia mitandao ya kijamii na njia zingine." Amesema Misime.
Polisi pia imetoa rai kwa kila mwananchi kuendelea kuungana kwa pamoja kulinda na kuimarisha amani na usalama wa Tanzania ili Taifa liendelee kuwa sehemu salama ya kuishi kwa vizazi vya sasa na vitakavyo kuja.

Social Plugin