Na Mwandishi wetu,Dar
Waziri wa Mambo ya ndani Mhe. George Boniface Simbachawene amesisitiza kuwa maandamano yanayohamasishwa kufanyika kesho Jumanne Disemba 09, 2025 ni haramu na yatadhibitiwa na Vyombo vya ulinzi na usalama ikiwa yatafanyika, akitaka wote wanaotaka kuandamana kufuata sheria na miongozo iliyopo.
Kulingana na Waziri Simbachawene mbele ya waandishi wa habari leo Jumatatu Disemba 08, 2025, amewaomba pia Watanzania kutojihusisha na maandamano hayo yasiyokuwa rasmi kisheria kutokana pia na kushamiri kwa matukio na viashiria vya uvunjifu wa amani na uhalifu.
"Maandamano hayo yanayoitwa ya amani hayaonekani yanaombwa na nani, kwa utaratibu gani na yatafanyika wapi. Haya yanayoelezwa ni kwamba wanaeleza tu kuwa yatakuwa hayana ukomo na yatakuwa makubwa kuliko yale ya tarehe 29."
"Ndugu zangu kama yakiwa hayo ni maandamano yasiyo na ukomo, maandamano ambayo ni makubwa kuliko yale ambayo watu walichoma mali za watu, watu, walichoma vituo vya mafuta, majengo ya serikali, Vituo vya polisi na hata watu wakafa, sasa haya tunayoambiwa ni makubwa kuliko yale si maandamano kwasababu kwanza hayana kibali kwa mujibu wa sheria lakini pia hayaeleweki yanafanywa na nani." Amesema Mhe. Waziri
Kulingana na Waziri Simbachawene, maandamano rasmi kulingana na sheria, maandamano ni lazima yawe na ukomo, lazima yaombwe na mtu mahususi, yawe na ujumbe, yaseme shabaha pamoja na kueleza muelekeo wake ili Jeshi la Polisi liweze kutoa huduma yake ya ulinzi kwa waandamanaji wa tukio husika.
Mhe. Simbachawene amethibitisha kuwa maandamano ya Disemba 09 ni haramu na yasiyokubalika, akitoa rai kwa wote walioichoka amani ya Tanzania kuheshimu sheria za nchi na ikiwa vinginevyo, Vyombo vya ulinzi na usalama vitawathibiti kulingana na sheria.



Social Plugin