Watanzania wamehimizwa kulinda na kuitunza miundombinu inayojengwa katika maeneo mbalimbali nchini ili iweze kudumu na kutumika kwa muda mrefu zaidi na kuwanufaisha zaidi, wakihimizwa pia kulinda amani kwa maslahi ya ustawi na maendeleo binafsi na ya Taifa kwa ujumla.
Wito huo umetolewa na Bi. Fatuma Ramadhan Mchekwa, Mkazi wa Temeke Jijini Dar Es Salaam wakati akizungumza na chombo chetu cha habari leo Jumanne Disemba 16, 2025, akisisitiza kuwa uharibifu wa Miundombinu umekuwa ukiligharimu taifa fedha nyingi.
"Tunachoomba sisi ni amani, amani iendelee na tusifanye fujo kwasababu tunapoharibu miundombinu ikiwemo ya mwendokasi hizi ni kodi zetu wenyewe kwahiyo tunajikomoa wenyewe. Tunafanya biashara tunalipa ushuru na kodi zetu ndizo zinazoleta maendeleo ila leo badala ya kusema tuendelee kuleta maendeleo tunarudi kukarabati miundombinu iliyoharibiwa." Amesema Bi. Fatuma.
Katika hatua nyingine Bi. Fatuma amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara ya Mbagala- Kariakoo, ujenzi wa shule ya msingi Kidugulo pamoja na kufikisha umeme kwenye maeneo yote ya Chanika, suala ambalo limeboresha maisha ya wananchi kupitia sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii.

Social Plugin