Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RC MAKALLA AANZA ZOEZI LA KUSIKILIZA KERO ZA WANANCHI KWA KUKUTANA NA WADAU WA BODABODA NA BAJAJI


Na Bora Mustafa, Arusha.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Amos Makalla, ameanza rasmi mchakato wa kusikiliza kero za wananchi wa Mkoa wa Arusha kwa kukutana na wadau wa usafirishaji wa bodaboda, bajaji pamoja na wananchi mbalimbali. Kikao hicho kimefanyika leo katika viwanja vya Makumbusho ya Azimio la Arusha.

 RC Makalla amesema lengo kuu ni kusikiliza changamoto zinazowakabili wananchi na kuzitafutia suluhisho la kudumu. Alibainisha kuwa kazi ya bodaboda na bajaji ni kazi halali kama kazi nyingine yoyote, na hivyo wahusika wake wanapaswa kuheshimiwa na kusaidiwa kwa njia rasmi.

Aidha, amesema changamoto zote zilizotolewa na viongozi wa vyama vya bodaboda na bajaji zitashughulikiwa kwa mpangilio na kushirikiana na kamati ya usalama ya mkoa. Amesisitiza umuhimu wa wadau hao kushirikiana na serikali pamoja na vyombo vya usalama barabarani kwa ustawi wa sekta hiyo.

Mhe. Makalla amezindua rasmi kampeni ya kusikiliza kero za wananchi, na kutoa agizo kwa wakuu wa wilaya kuanza mikutano ya hadhara katika maeneo yao ili wananchi wapate fursa ya kueleza matatizo yao moja kwa moja.

Kwa upande wake, Katibu wa umoja wa bodaboda Jiji la Arusha, Khatibu Msemo, amesema sekta ya bodaboda inachangia kukuza utalii wa ndani na nje ya nchi. Aidha, alisema kazi hiyo inasaidia familia na kaya kupata kipato cha kila siku, huku wakijitahidi kudumisha nidhamu na kuimarisha usalama.

Khatibu ameeleza kuwa kwa kushirikiana na ofisi ya Mkuu wa Mkoa, wameweza kupunguza vitendo vya kihalifu, na kwa sasa wamefanikiwa kuwaingiza wanachama kwenye mfumo rasmi wa taarifa (database). Hata hivyo, alitaja changamoto kama ukosefu wa barabara nzuri, sare rasmi kwa waendesha bodaboda, na ukosefu wa maendeleo endelevu ya sekta hiyo.

Mmoja wa wadau wa bodaboda, anayefahamika kwa jina la Msukuma, alilalamikia uwepo wa pikipiki zenye kelele kubwa na taa za “disko”, akisisitiza haja ya ushirikiano ili kudhibiti hali hiyo kwa usalama wa wote.

Aidha, mmoja wa wawakilishi wa bajaji alisema walipata changamoto za awali kama mgomo wa madereva kwa madai kuwa bajaji zimezidi mjini. Hata hivyo, tatizo hilo liliwahi kushughulikiwa. Hata hivyo, aliomba serikali kuwarejeshea baadhi ya vituo vya kazi walivyohamishwa, ili waweze kuendelea na shughuli zao kwa utaratibu rasmi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com