Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KAMPENI YA SIKU 16 TCRS YAIMARISHA ULINZI WA MTOTO WA KIKE KISHAPU


Baadhi ya wanafunzi wa kidato cha tatu shule ya sekondari Mwakipoya iliyoko Kata ya Mwakipoya wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga wakifurahia elimu ya hedhi salama na kupokea taulo za kike kutoka shirika la TCRS shuleni hapo Disemba 5,2025

Na Sumai Salum – Kishapu

Shirika la Tanganyika Christian Refugee Service (TCRS) limeendelea kuonyesha dhamira yake ya kuinua na kulinda haki za wasichana, baada ya kugawa taulo za kike 104 kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mwakipoya, Kata ya Mwakipoya, Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga.

Zoezi hilo limefanyika leo Disemba 5,2025 ambapo wanafunzi wa kike wamepewa elimu ya hedhi salama, pamoja na uelewa kuhusu kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia, inayoadhimishwa kila mwaka kuanzia Novemba 25 hadi Desemba 10 duniani kote.

Akizungumza wakati wa tukio hilo, Mratibu wa Mradi wa TCRS Kata ya Mwakipoya, Emmanuel Samwel, amesema kampeni ya siku 16 ni muhimu katika kuongeza uelewa wa jamii kuhusu ukatili unaowakumba watoto wa kike na wanawake.

“Kupitia kampeni hii tumejipanga kuhakikisha tunawawezesha watoto wa kike kupata uelewa, ujasiri na vifaa vinavyowawezesha kushinda vikwazo vinavyosababishwa na ukatili wa kijinsia. Taulo hizi za kike ni sehemu ya jitihada za kuwaondoa kwenye hatari ya kukosa masomo au kukumbana na dharau wakati wa hedhi,” amesema Samwel.

Aidha, Mwezeshaji wa mada ya Hedhi Salama na Mratibu msaidizi wa afya ya uzazi na mtoto Wilayani humo, Rehema Jumanne, amewasilisha somo kuhusu umuhimu wa usafi wa hedhi, akisisitiza kuwa kutunza mwili wakati wa hedhi si suala la hiari bali ni haki ya kiafya kwa kila mtoto wa kike.

“Hedhi salama huongeza kujiamini, hupunguza maambukizi na husaidia mtoto wa kike kuhudhuria masomo bila hofu. Tunawaelimisha ili wajue hedhi si aibu, na wajenge ujasiri wa kukabiliana na maisha,” ameongeza Rehema.

Walimu wa shule hiyo wametoa pongezi kwa TCRS kwa mchango wao wa kuimarisha afya na ustawi wa wanafunzi, huku wakitoa wito kwa wazazi na jamii kuendelea kushirikiana kupinga ukatili wa kijinsia na kuunga mkono mahitaji ya mtoto wa kike.

Kampeni hii ya TCRS inaendelea katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Kishapu kwa lengo la kulinda heshima, afya na ndoto za wasichana.

Mratibu wa Mradi wa TCRS Kata ya Mwakipoya, Emmanuel Samwel akielezea umuhimu wa kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia katika kuongeza uelewa wa jamii kuhusu ukatili unaowakumba watoto wa kike na wanawake akizungumza na wanafunzi wa kike kidato cha pili,tatu na nne wa shule ya Sekondari Mwakipoya Disemba 5,2025 zoezi lililoratibiwa na kuwezeshwa na TCRS mkoani humo
Mwezeshaji wa mada ya Hedhi Salama na Mratibu msaidizi wa afya ya uzazi na mtoto wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, Rehema Jumanne akielezea umuhimu na faida za hedhi salama kwa wanafunzi wa kike kidato cha pili,tatu na nne wa shule ya Sekondari Mwakipoya Disemba 5,2025 zoezi lililoratibiwa na kuwezeshwa na TCRS mkoani humo























Picha ya pamoja ya wawezeshaji na wanafunzi waliohitimu kidato cha nne shule ya Sekondari Mwakipoya iliyoko Kata ya Mwakipoya wilaynai Kishapu mkoani Shinyanga

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com