Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DC NKINDA ACHUKUA HATUA ZA HARAKA KUTATUA KERO YA BARABARA MHONGOLO NA NYASHIMBI, KAHAMA



Na Neema Nkumbi, Kahama

Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mhe. Frank Nkinda, amechukua hatua za haraka kutatua changamoto ya miundombinu ya barabara katika mitaa na kata mbalimbali za Manispaa ya Kahama, kufuatia kero zilizowasilishwa na vijana wakati wa sherehe za Krismasi walipokutana naye kwa chakula cha pamoja.

Leo Desemba 31, 2025, DC Nkinda ametembelea Mtaa wa Mhongolo ambapo amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyoyatoa katika hotuba yake wakati wa uzinduzi wa Bunge la 13, akiwataka watumishi wa umma kuwahudumia wananchi kwa vitendo na kuwaletea tabasamu wale waliomwamini na kumpa ridhaa ya kuwaongoza.

Akizungumza na waandishi wa habari, Nkinda amesema Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kahama imefanikiwa kutafuta mtambo wa kuchonga barabara (greda) ili kuanza kushughulikia kero za barabara zilizoharibika katika maeneo mengi kutokana na mvua, akisisitiza kuwa lengo ni kuhakikisha wananchi hawakwami katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku, hususan shughuli za kujipatia kipato.

“Ninatoa shukrani zangu kwa Mheshimiwa Rais, kwani Serikali imetutengea fedha kwa ajili ya kumaliza changamoto ya miundombinu ya barabara, Hata hivyo, Ofisi ya Mkuu wa wilaya Kahama imeona ichukue hatua za haraka wakati tukiendelea kusubiri fedha hizo kutufikia,” amesema Nkinda.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyashimbi, Kata ya Mhongolo, Emanuel Lutonja, amemshukuru Rais Samia pamoja na DC Nkinda kwa hatua hiyo, akisema ujio wa greda katika mtaa wake umepunguza kwa kiasi kikubwa kero za barabara zilizokuwa na madimbwi makubwa yaliyowaathiri wafanyabiashara, hususan bodaboda, bajaji na wajasiriamali walioko pembezoni mwa barabara.

“Barabara hii ni kiunganishi kikuu kati ya Nyashimbi, Mhongolo hadi mjini, hivyo ukarabati wake utasaidia sana wananchi wa mtaa huu kufanya kazi zao bila wasiwasi,” amesema Lutonja.

Naye Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Mhongolo, Renatus Thomas, amesema jitihada za DC Nkinda zinastahili pongezi, akibainisha kuwa bila uongozi wake barabara hiyo isingetengenezwa kwa wakati hivyo amemuomba DC kuendelea na zoezi hilo kwani barabara nyingi za Mhongolo bado ni mbovu na zina madimbwi makubwa.

Mkazi wa Nyashimbi Sokoni, Japhet Kitima, amesema awali wafanyabiashara walipata changamoto kubwa kuingiza mizigo kwa magari kutokana na ubovu wa barabara, hali iliyosababisha hasara hivyo wanamshukuru DC kwa kuwaletea greda kwani sasa hali imeanza kubadilika.

Kwa upande wake, Zainabu, mkazi wa Mhongolo na mfanyabiashara wa chakula, amesema mashimo na matope yaliyokuwapo barabarani yalikuwa yakisababisha usumbufu mkubwa hasa magari yalipopita, huku mkazi mwingine wa Nyashimbi, Sharifa Ramadhan, ameeleza kuwa maji yaliyotuama barabarani yalikuwa yakirukia madukani mwao na kutoa harufu mbaya, hali iliyosababisha hata bajaji za mizigo kukataa kufika eneo hilo.

Sambamba na ukarabati wa barabara, DC Nkinda amewataka viongozi wa mitaa ya Mhongolo na Nyashimbi kuhakikisha mitaro iliyoziba kwa mchanga inazibuliwa ili kuruhusu maji kupita vizuri, akibainisha kuwa kuziba kwa mitaro ndiko chanzo kikuu cha uharibifu wa barabara nyingi.

Katika ziara hiyo, DC Nkinda ametembelea barabara ya Mhongolo Senta kuelekea KACU pamoja na barabara ya Mhongolo kuelekea Nyashimbi Sokoni, akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kushughulikia kero za wananchi kwa vitendo na kwa wakati.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com