Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TUME YA MADINI, TRA ZAUNGANISHA NGUVU KUONGEZA UFANISI WA UKUSANYAJI MADUHULI


DODOMA

TUME  ya Madini kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) zimeimarisha ushirikiano wao kwa lengo la kuongeza ufanisi na tija katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi hizo, hususan katika ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali yatokanayo na shughuli za madini.

Akifungua kikao kazi cha kuhuisha Mkataba wa Makubaliano (MoU) leo Desemba 18, 2025 katika Ukumbi wa Tanzanite uliopo Ofisi za Tume ya Madini jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Tume ya Madini, Nsajigwa Kabigi, amesema ushirikiano huo unatarajiwa kuleta matokeo chanya katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi hizo kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

Amesema MoU hiyo inalenga kuimarisha ushirikiano kupitia ubadilishanaji wa taarifa, mafunzo ya pamoja na utekelezaji wa kaguzi za pamoja, hatua itakayoongeza uwazi, ufanisi na tija katika ukusanyaji wa maduhuli yanayotokana na shughuli za Sekta ya Madini.

“Kwa kutambua mchango mkubwa wa TRA katika kufanikisha majukumu ya Serikali, Tume ya Madini iliona umuhimu wa kuimarisha ushirikiano huu kupitia MoU itakayowezesha kubadilishana taarifa, kufanya mafunzo na kaguzi za pamoja,” amesema Kabigi.

Aidha, amebainisha kuwa Serikali inatambua umuhimu wa taasisi zake kushirikiana kwa karibu, akirejea maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyeagiza mifumo ya Serikali kusomana mapema ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuongeza upatikanaji wa taarifa miongoni mwa taasisi za umma.

“Ninatambua kikao hiki kitaanzisha Kamati ya Pamoja na Kamati ya Ufundi; nawasisitiza watakaoteuliwa kutekeleza majukumu yao kwa weledi na uwajibikaji ili kuhakikisha malengo ya ushirikiano huu yanafikiwa,” ameongeza.

Kadhalika, Kabigi amesisitiza umuhimu wa majadiliano yenye tija yatakayozalisha maazimio madhubuti, yatakayosaidia kuimarisha utendaji wa taasisi hizo na kuchangia maendeleo ya Sekta ya Madini pamoja na taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Meneja wa TRA Mkoa wa Dodoma, Pendolake Elinisafi, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Tume ya Madini na TRA, akieleza kuwa Mamlaka hiyo imeendelea kuboresha mifumo ya TEHAMA, hususan matumizi ya Electronic Fiscal Devices (EFDs), pamoja na kutoa elimu ya kodi kwa wadau ili kujenga mazingira rafiki ya ukusanyaji wa mapato kupitia mazungumzo na ushirikiano wa karibu kati ya taasisi husika.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com