
Kamati ya Wataalamu wa Masuala ya Habari Zanzibar (ZAMECO) imeungana na wanaharakati, wanahabari na watetezi wa haki za binadamu duniani kuadhimisha Siku ya Haki za Binadamu ambayo hufanyika kila Desemba 10.
Katika maadhimisho ya mwaka huu yanayobeba kaulimbiu “Mahitaji ya Kila Siku”, ZAMECO imesisitiza umuhimu wa kulinda haki za msingi za binadamu, ikiwemo uhuru wa kupata na kutoa taarifa—ikiwa ni nguzo muhimu ya utawala bora na demokrasia.
Kwa mujibu wa taarifa yao kwa vyombo vya habari, ZAMECO imesisitiza kuwa haki ya kupata taarifa sahihi, kuhoji, kushiriki na kuwawajibisha watawala ni wajibu wa msingi wa jamii yoyote inayolinda misingi ya haki za binadamu. Taarifa hiyo imekumbusha pia umuhimu wa Tamko la Ulimwengu la Haki za Binadamu (UDHR) la 1948 ambalo linatambua uhuru wa habari kama msingi wa ushiriki wa wananchi katika masuala ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.
Hata hivyo, ZAMECO imeeleza kuwa licha ya misingi hiyo iliyo wazi, tasnia ya habari Zanzibar bado inakabiliwa na vikwazo vinavyoathiri utekelezaji wa haki hizi. Vikwazo hivyo vinatajwa kuwa ni pamoja na mazingira ya hofu, vitisho dhidi ya waandishi, ucheleweshaji wa taarifa za umma pamoja na matumizi ya sheria kandamizi ambazo zimepitwa na wakati.
Aidha, ZAMECO imetoa wito kwa Serikali ya Zanzibar kufanya mapitio ya sheria zote zinazosimamia habari ili ziendane na mazingira ya sasa ya kidemokrasia, maendeleo ya teknolojia, na matakwa ya Katiba pamoja na viwango vya kimataifa.




Social Plugin