Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Dodoma limetoa hadhari makundi mitandaoni yanayochochea vurugu, huku likisisitiza umuhimu wa kudumisha amani na utulivu wa nchi.Mwenyekiti wa BAKWATA, Wilaya ya Dodoma, Sheikh Bashiru Ghazali, akizungumza kwa uzito, amesema makundi haya yanatumia mitandao kwa nia ya "kusababisha ubaguzi dhidi ya viongozi na serikali".
Kauli hii inalingana na maoni ya wananchi. Mzazi Aisha Kayuni wa Mbeya anayesisitiza kuwa, “Taasisi za kiserikali hazipaswi kutoa fursa kwa taasisi za kidini kuhubiri na kuonesha chuki, uhasama wala kuwalaumu waumini wao”.
Wananchi wanaaswa kuwa makini na kuepuka kufuata ajenda za vikundi hivi.
Mzazi Samwel Ali anatoa wito, akisisitiza “amani ndio chanzo cha furaha na ustawi wangu binafsi”. .
Hivi karibuni Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene, amesikika akisema inapaswa kuwa na kengele ya kuamsha kila kijana wa Kitanzania anayeipenda Nchi hii akitafakari methali isemayo, "Akipenda chongo, huita kengeza," lakini linapokuja suala la amani ya nchi, hatuna anasa ya kujidanganya.
Akirejea mfano wa jirani zetu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Waziri alituonyesha picha halisi na ya kutisha: Taifa ambalo limekuwa kwenye migogoro kwa zaidi ya miaka 30. Vijana wa huko, ambao leo ni wazee, wamepoteza maisha yao yote wakitafuta amani ambayo walichezea miongo mitatu iliyopita.
Kwa kijana "Gen Z" unayesoma hapa: Hii amani tuliyonayo siyo zawadi, ni jukumu. Wale wanaokushawishi uingie barabarani kubomoa maduka na kuchoma matairi hawatakuwepo wakati uchumi unaporomoka. Hawatakuwepo wakati mama lishe anashindwa kuuza chakula au bodaboda anashindwa kupata abiria kwa hofu ya usalama.
Tanzania ni kisiwa cha amani katika bahari iliyojaa dhoruba. Tumeona kilichotokea Sudan, tumeona Kongo. Njia ya mkato ya vurugu haijawahi kumfikisha mtu kwenye neema. Njia pekee ya kweli ni ile ya kujenga,kujenga hoja mezani, na kujenga taifa kwa kufanya kazi.
Tusiiingize nchi kwenye umwagaji damu kwa majaribio yasiyo na tija. Amani ni kama afya—ukiipoteza ndipo utajua thamani yake. Tuitunze, tuilinde, na tuiheshimu kwa vitendo.
Social Plugin