Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

POLISI DODOMA: TUTACHUNGZA KILICHOMUUA MC PILIPILI




Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Jeshi la Polisi nchini limetia pole kwa Tasnia ya burudani nchini baada ya kupata mshtuko mkubwa kufuatia kifo cha mchekeshaji maarufu, Emmanuel Mathias Matebe, anayejulikana zaidi kama MC Pilipili, ambaye amefariki dunia Novemba 16, 2025 katika Kituo cha Afya Ilazo, jijini Dodoma.

Kwa mujibu wa maelezo ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma, yaliyotolewa Novemba 19, 2025 na Kamishna Msaidizi wa Polisi William Mwamafupa, marehemu aliletwa kituoni hapo na watu aliowaita “wasiokuwa wakijulikana” akiwa katika hali mbaya kiafya kabla ya kuthibitishwa kufariki dunia majira ya saa 9:00 alasiri.

Taarifa zinaeleza kuwa kabla ya tukio hilo, majira ya saa 8:00 mchana, msaidizi wa MC Pilipili, Hassan Ismail, alipokea simu kutoka kwa mtu asiyejulikana akimtaka kufika eneo fulani kwa mazungumzo. Baadaye, gari dogo jeupe lilifika likiwa na MC Pilipili ambaye alionekana kuchoka na akiwa na majeraha. Watu waliokuwa kwenye gari hilo walimshusha na kuondoka bila kutoa maelezo.

Tathmini ya awali iliyofanywa na wataalamu wa afya kwa kushirikiana na Polisi imebaini kuwa marehemu alipata majeraha sehemu mbalimbali za mwili yanayoashiria kushambuliwa kabla ya kufariki dunia.

Polisi wamesema kuwa uchunguzi wa kina unaendelea kubaini kilichotokea hadi kufikia kifo hicho, pamoja na kuwatafuta waliohusika ili sheria ichukue mkondo wake.

Kifo cha MC Pilipili kimeibua simanzi na majonzi makubwa kwa mashabiki na wasanii wenzake, wengi wao wakimiminika mitandaoni kutuma salamu za rambirambi na kuhoji mazingira yaliyopelekea kifo chake.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com