Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeendelea kuhimiza urasimishaji wa vikundi vya huduma ndogo za fedha (VICOBA) kama njia ya kuhakikisha usalama wa fedha na uwazi wa shughuli za vikundi.
Wataalamu wa benki hiyo wanasema hatua hiyo inaweza kuongeza imani ya wanachama na kutoa ulinzi wa kisheria pale panapojitokeza changamoto au migogoro ndani ya vikundi, jambo linalowapa wanachama amani ya kutumia mfumo huu kwa maendeleo ya familia zao.
Meneja Usimamizi wa Watoa Huduma Ndogo za Fedha wa BoT, Dickson Gama, ameeleza kuwa licha ya VICOBA kuwa chanzo muhimu cha mitaji kwa wananchi wa kipato cha chini, changamoto za usimamizi na ukosefu wa uwazi bado zinahatarisha uaminifu wa wanachama.
Baadhi ya vikundi vimekuwa vikikosa kurasimishwa kwa muda mrefu, jambo linalosababisha malalamiko kuhusu matumizi yasiyoeleweka ya fedha na upendeleo katika utoaji mikopo, na hivyo kudhoofisha mshikamano wa kijamii ndani ya vikundi.
Gama amebainisha kuwa ukosefu wa uwazi wa baadhi ya viongozi unachangia migogoro, kwani maamuzi mengi hufanywa bila kushirikisha wanachama.
Aidha,ameeleza kuwa upungufu wa takwimu sahihi na uhaba wa taarifa unaleta changamoto kubwa kwa usimamizi, huku ukizuia wadhibiti na serikali za mitaa kufanya tathmini sahihi kuhusu maendeleo ya vikundi hali inaweza kudhoofisha usalama wa fedha zinazotegemewa na kaya nyingi.
Ili kuboresha hali hiyo,amesema Serikali kupitia TAMISEMI imepewa jukumu la kusimamia mchakato wa urasimishaji, ikiwemo kupokea maombi kupitia mfumo wa WEZESHA PORTAL, kutunza rejista ya vikundi vilivyosajiliwa na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara.
" Kanuni zinazoongoza sekta hiyo zinataka vikundi vipya kuwa na wanachama 10–50, kufanya mkutano wa awali wa kuchagua kamati ya muda, na kuendesha mkutano wa uanzishaji chini ya afisa aliyeidhinishwa, hatua zinazohakikisha msingi imara wa uongozi na uwajibikaji kabla ya kuanza shughuli rasmi, "ameeleza
Aidha amesema baada ya kusajiliwa, vikundi vinatakiwa kuanza shughuli ndani ya miezi mitatu, kuwa na ofisi rasmi, kufungua akaunti ya benki, kutunza rekodi sahihi za fedha na kuwasilisha taarifa za robo mwaka.
Amefafanua kuwa BoT na TAMISEMI wana mamlaka ya kufanya ukaguzi wa ghafla ili kulinda maslahi ya wanachama na kuzuia matumizi mabaya ya fedha. Hatua hizi zinalenga kuhakikisha sekta ya VICOBA inakuwa imara, salama na yenye manufaa kwa wananchi wanaotegemea mfumo huo kujikwamua kiuchumi na kuimarisha familia zao.



Social Plugin